Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA) imewataka wakulima kutumia teknolojia za kisasa za uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ili kupunguza upotevu, kuhifadhi virutubishi na kuongeza kipato, ikiwemo teknolojia ya uchakataji wa mchele joto inayotumia mvuke.

Teknolojia hiyo imeoneshwa katika banda la NAESA wakati wa maonesho ya kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Tanga, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, alitembelea banda hilo kujionea ubunifu mbalimbali unaolenga kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani ya Mazao wa NAESA, Bi. Esther Mwaisango, amesema wakala huo una jukumu la kuratibu na kusimamia huduma za ugani, ikiwemo kuwawezesha maafisa ugani kupata maarifa na teknolojia zitakazowasaidia kuwafikishia wakulima elimu sahihi ya kilimo.

Amesema katika maonesho hayo, NAESA imeshirikisha wakufunzi kutoka vyuo vitano vya mafunzo ya kilimo, wakiwemo wa MATI Uyole, Mlingano, Mubondo na Ilonga, ambao wameonesha teknolojia mbalimbali zinazoweza kutumika kuongeza thamani ya mazao na kukidhi mahitaji ya soko.

Ameongeza kuwa kupitia mafunzo na usambazaji wa teknolojia hizo kwa maafisa ugani, wakulima wataweza kupata elimu ya vitendo itakayowasaidia kuboresha namna ya kuchakata, kuhifadhi na kuuza mazao yao kwa tija zaidi.

Kwa upande wake, mkufunzi kutoka Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo (MATI Ilonga), kilichopo Kilosa mkoani Morogoro, Bw. Hamis Abdalah Ramadhani, amesema teknolojia ya uchakataji wa mchele joto (parboiling) kwa kutumia mvuke imebuniwa ili kuongeza thamani ya mpunga, kupunguza upotevu wa virutubishi na kumwezesha mkulima kupata bei nzuri zaidi sokoni.

Amesema teknolojia hiyo inahusisha hatua za kuandaa mpunga kabla ya kukobolewa, ambapo huhifadhiwa kwa muda unaofaa na kufanyiwa uchakataji kwa kutumia mvuke, hatua inayosaidia virutubishi kutoka katika tabaka la nje kuelekea ndani ya punje ya mchele.

Ameeleza kuwa utaratibu huo husaidia kupunguza kuvunjika kwa punje wakati wa ukoboaji na kuhifadhi virutubishi muhimu, hivyo kumwezesha mkulima kupata mchele wenye ubora unaoweza kuongeza ushindani wake sokoni.

Ramadhani amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kumsaidia mkulima kuachana na uuzaji wa mpunga ghafi kwa bei ya chini na badala yake kuongeza thamani ya mazao yake kupitia uchakataji, jambo linaloweza kuboresha kipato na kuimarisha maisha yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amepongeza teknolojia mbalimbali za kilimo zilizooneshwa katika maonesho hayo, akisema matumizi ya teknolojia bora ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi, hususan wakulima, kutumia fursa za maonesho hayo kujifunza teknolojia mpya na kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi bora katika shughuli zao za kilimo.

Maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika mnyororo wa thamani wa mazao, kuanzia uzalishaji hadi uchakataji na masoko, kwa lengo la kuongeza tija, kupunguza upotevu wa chakula na kuboresha kipato cha wakulima.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...