Na Mwandishi Wetu, Chamwino – Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi kampeni za mgombea wake wa ubunge katika Jimbo la Chamwino, Dkt. Nettho Ndilito, huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akiwaomba wananchi kumchagua kwa kishindo ili aendelee kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo.
Uzinduzi wa kampeni hizo umefanyika leo, Oktoba 16, 2026, katika Kijiji cha Dabalo, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM pamoja na wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ndejembi, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amewataka wananchi wa Chamwino kumpigia kura Dkt. Ndilito ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta za huduma za kijamii, zikiwemo maji, umeme, barabara, elimu na afya.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, hivyo amewahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kumchagua mgombea wa CCM.
Ndejembi amewataka pia wagombea wote walioshiriki mchakato wa ndani wa chama hicho kuungana na wanachama wengine ili kumuunga mkono Dkt. Ndilito katika kampeni hizo.
Makamu huyo wa Rais, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Chamwino, amewaahidi wananchi kuendelea kushirikiana nao katika juhudi za kuhakikisha jimbo hilo linapata maendeleo yaliyokusudiwa.
Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua za maendeleo zilizotekelezwa katika jimbo hilo na kuwataka wananchi kuendelea kumuombea katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuliongoza taifa.
Ndejembi pia amewashukuru wananchi wa Chamwino kwa ushirikiano waliompa wakati wote alipokuwa akilihudumia jimbo hilo kama mbunge, akisema anathamini mchango wa kila mmoja katika kufanikisha maendeleo ya eneo hilo.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM, wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wabunge, madiwani na wananchi wa Jimbo la Chamwino.
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...