Na Mwandishi Wetu, Simanjiro
Kero 102 zimeibuliwa na wananchi katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, James Ole Millya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kilichofanyika Orkesumet, Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo, Frank Oleleshwa, amesema kero hizo ziliibuliwa wakati wa ziara iliyohusisha kata za Emboreet, Loiborsiret na Komolo.
Oleleshwa amesema katika ziara hiyo, Mbunge Ole Millya alikutana na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kujadiliana nao kuhusu namna ya kuzitatua.
Amesema kabla ya kuendelea na mikutano ya wananchi, mbunge huyo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Emboreet, ambako alizungumza na wanafunzi pamoja na baadhi ya wananchi wa kata hiyo.
Baadaye, Ole Millya alitembelea Kijiji cha Kimotorok kilichopo Kata ya Loiborsiret, ambako alisikiliza kero za wananchi na kuzungumza nao, kabla ya kuendelea na ziara katika Kijiji cha Loiborsiret na kuhitimisha shughuli zake Kata ya Komolo.
Oleleshwa amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, kwa kuwezesha upatikanaji wa basi na watumishi wa halmashauri, wakiwemo wakuu wa idara na vitengo, walioshiriki katika ziara hiyo ili kusaidia kutoa ufafanuzi na majibu kuhusu changamoto za wananchi.
Amesema miongoni mwa kero 102 zilizowasilishwa ni migogoro ya ardhi, uhitaji wa ukarabati wa baadhi ya barabara, pamoja na ukosefu wa huduma ya umeme na maji katika baadhi ya vitongoji.
Aidha, amesema wananchi wameeleza hofu yao kutokana na tembo kuvamia makazi katika baadhi ya vijiji na kuhatarisha usalama wao.
Kuhusu changamoto hiyo, Oleleshwa amesema mbunge alishauri kujengwa kwa mabwawa ya maji karibu na maeneo ya hifadhi ili kusaidia kupunguza uhitaji wa tembo kutoka maeneo hayo kwenda kutafuta maji katika makazi ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Oleleshwa amesema Ole Millya, ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi katika ziara ya kitaifa akiwa katika nafasi yake ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amemtuma kufikisha salamu zake kwa wajumbe wa Baraza la Madiwani.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...