Na Seif Mangwangi, Michuzi TV Kilimanjaro


BENKI ya Dunia imezitaka kampuni na taasisi zinazotekeleza miradi ya uzalishaji umeme nchini na nje ya Tanzania kutumia wataalamu wazawa wanaopatiwa mafunzo katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), ikieleza kuwa mradi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa maji Kikuletwa utakaokamilika Desemba mwaka huu utakuwa fursa muhimu ya kuwaandaa wataalamu hao kwa soko la ajira.

Akizungumza Oktoba 29, 2026 wakati wa ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia kukagua maendeleo ya mradi huo, Nkahiga Kaboko, Mtaalamu Mwandamizi wa Elimu na Ukuzaji Ujuzi wa Benki ya Dunia, Ofisi ya Dar es Salaam, ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Miradi ya Elimu ya Ufundi na Elimu ya Juu inayofadhiliwa na benki hiyo, amesema wataalamu wa ATC wanajengewa uwezo wa kutosha katika teknolojia ya uzalishaji umeme wa maji.

Kaboko amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha wanafunzi na walimu wa chuo hicho kupata mafunzo ya vitendo katika mazingira halisi ya uzalishaji umeme, hatua itakayosaidia kuimarisha ujuzi wao na kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa.

Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na taasisi mbalimbali za elimu ya ufundi kutekeleza mradi huo, akisema uwekezaji katika ujuzi ni muhimu katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuwawezesha vijana kujipatia kipato kupitia taaluma walizosomea.

Amesema mradi huo umehusisha ushirikiano wa taasisi mbalimbali za elimu ya ufundi, zikiwemo ATC, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ambazo zimekuwa zikijenga uwezo wa walimu na wataalamu katika teknolojia mbalimbali za kisasa.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamehusisha wataalamu katika ngazi mbalimbali za elimu, kuanzia diploma hadi shahada za juu, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na rasilimali watu wenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati bila kutegemea kwa kiwango kikubwa wataalamu kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wa utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Isaac Laganda, mmoja wa wataalamu wanaosimamia ujenzi wa mtambo huo, amesema kazi zinaendelea vizuri huku kifurushi cha kwanza kinachohusisha ufungaji wa mitambo ya kuzalisha umeme, ikiwemo propela na mifumo ya udhibiti (control panels), kikifikia hatua ya mwisho ya ukamilishaji kwa takribani asilimia 99.

Amesema kifurushi cha pili kinachohusisha kazi za ujenzi wa miundombinu (civil works), ikiwemo ujenzi wa mifumo ya kuelekeza na kuingiza maji katika mtambo, kimefikia takribani asilimia 45 ya utekelezaji.

Laganda amesema mtambo huo utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha megawati 1.6 za umeme, ambao utachangia upatikanaji wa nishati kwa matumizi mbalimbali na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

Akizungumza maandalizi ya mvua za Elnino, amesema katika utekelezaji wa mradi huo, wataalamu wamezingatia pia masuala ya usalama wa miundombinu kwa kujenga kingo na mifumo maalumu ya kudhibiti maji ili kuhakikisha yanaelekezwa kwenye maeneo yaliyokusudiwa bila kuhatarisha mtambo na miundombinu yake.

Amesisitiza kuwa mradi huo unaonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania katika teknolojia ya uzalishaji umeme kwa kutumia maji (Hydropower), akibainisha kuwa wahandisi wazawa wameshiriki moja kwa moja katika kazi za usimamizi na utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na wataalamu wengine.

Kwa upande wake, Dkt. Fredrick Salukele, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Mratibu wa Mradi wa EASTRIP kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, ameipongeza Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kutekeleza mradi huo unaolenga kuimarisha elimu ya ufundi na kujenga uwezo wa wataalamu wa Kitanzania.

Salukele amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha elimu ya ufundi inakwenda sambamba na mahitaji ya sekta za uzalishaji, kwa kuwa vijana wanahitaji kupata ujuzi unaowawezesha kushiriki moja kwa moja katika miradi ya maendeleo na kupata ajira.

Amesema mradi wa Kikuletwa ni mfano wa uwekezaji unaounganisha mafunzo ya darasani na vitendo, ambapo walimu na wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza kuhusu usanifu, ujenzi, ufungaji na uendeshaji wa mitambo ya kuzalisha umeme.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika kuimarisha taasisi za elimu ya ufundi kwa kuzipatia vifaa na miundombinu ya kisasa ya kufundishia, ili wahitimu waweze kukidhi viwango vya ujuzi vinavyohitajika katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt Mussa. Chacha amesema chuo hicho kimefurahi kupokea ujumbe wa Benki ya Dunia pamoja na viongozi wa Wizara ya Elimu kwa ajili ya kujionea maendeleo ya mradi huo, akieleza kuwa ni sehemu muhimu ya juhudi za kuimarisha elimu ya ufundi nchini.

Amesema mradi huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kujenga uchumi imara unaotegemea viwanda, teknolojia na ubunifu, mambo ambayo yanahitaji upatikanaji wa nishati ya uhakika pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa kisasa.

Ameeleza kuwa ukuaji wa viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi unahitaji umeme wa kutosha, hivyo ni muhimu kuwekeza katika uzalishaji wa nishati sambamba na kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kutumia, kusimamia na kuendeleza teknolojia za kisasa za uzalishaji umeme.

Amesema mradi huo hautakuwa miundombinu ya kuzalisha umeme pekee, bali pia utakuwa eneo muhimu la mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na walimu wa ATC, hatua itakayosaidia kuzalisha wataalamu wenye uzoefu unaohitajika katika sekta ya nishati.

Ametoa wito kwa vijana kutumia fursa za mafunzo ya ufundi na teknolojia zinazotolewa na taasisi mbalimbali nchini, akisisitiza kuwa ujuzi wa vitendo ni nyenzo muhimu ya kujiajiri, kuajiriwa na kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo.

Mradi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa maji Kikuletwa ni sehemu ya uwekezaji unaotekelezwa kupitia mradi wa EASTRIP kwa lengo la kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, huku ukitarajiwa kuchangia upatikanaji wa nishati na kujenga kizazi cha wataalamu wa Kitanzania wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...