Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imewataka wataalamu wa fani hiyo kukamilisha malipo ya ada za uanachama kwa wakati, ikionya kuwa wanaoshindwa kulipa kwa kipindi cha miezi 24 wanaweza kufutiwa usajili na kupoteza sifa za kufanya kazi katika sekta ya umma na binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo  jijini Dodoma, Mkurugenzi wa PSPTB, Godfrey Mbanyi, amesema bodi imesajili jumla ya wataalamu 22,269 katika ngazi mbalimbali, lakini ni 4,449 pekee walio katika kundi la wanachama hai baada ya kutimiza masharti ya uanachama, ikiwemo kulipa ada na kutokuwa na madeni.

Mbanyi amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 38 ya Kanuni za Bodi, mtaalamu atakayeshindwa kulipa ada za uanachama kwa kipindi cha miezi 24 anaweza kufutiwa usajili. Ameeleza kuwa hatua hiyo ina athari kubwa kwa mtaalamu husika, kwani kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB, Sura ya 179 ya mwaka 2007, hatakuwa na sifa za kutekeleza majukumu ya kitaaluma katika eneo la ununuzi na ugavi.

Amesema hali hiyo inaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, hasa pale mtaalamu anayehusika na hatua muhimu za mchakato wa ununuzi wa umma anapopoteza sifa za kitaaluma na kushindwa kuendelea na majukumu yake.

Kwa mujibu wa Mbanyi, takribani wataalamu 18,220 bado hawajafikia hadhi ya kuwa wanachama hai, wakiwemo wale wenye madeni ya ada. Hata hivyo, baadhi yao wameanza kufanya malipo, huku wengine wakiahidi kukamilisha madeni yao kabla ya Desemba 31, 2026.

Amesema bodi inaendelea kuwasiliana na wataalamu hao kupitia barua pepe, simu na barua rasmi kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wao wa kulipa ada. Kwa wale ambao hawajaonyesha nia ya kutekeleza wajibu huo, bodi imepanga kushirikisha waajiri wao ili kuhakikisha malipo yanafanyika na kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika utendaji wa taasisi.

Aidha, Mbanyi amebainisha kuwa kufanya kazi bila kuwa mwanachama hai kunaweza kumnyima mtaalamu na mwajiri wake baadhi ya haki za kitaaluma, ikiwemo kupata msaada wa bodi katika kushughulikia malalamiko na migogoro ya kinidhamu inayohusiana na utekelezaji wa majukumu ya ununuzi na ugavi.

Ameonya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha hasara kwa taasisi za umma na binafsi, hususan pale mtaalamu anapotoa ushauri usio sahihi wa kitaaluma na mwajiri akashindwa kupata msaada unaostahili kutoka kwa bodi.

Katika hatua nyingine, Mbanyi amesema PSPTB itaweka kwenye tovuti yake orodha ya wanachama hai na kuisasisha kila Ijumaa ili kujumuisha wataalamu watakaokamilisha malipo ya madeni na kutimiza masharti ya usajili.

Ameongeza kuwa bodi inaendelea kuboresha mifumo yake ya taarifa za wanachama ili kuhakikisha taarifa zinakuwa sahihi na kurahisisha uthibitishaji wa sifa za kitaaluma za wataalamu wa ununuzi na ugavi.

Mbanyi amewahimiza wataalamu pamoja na waajiri wao kushirikiana kuhakikisha ada za uanachama zinalipwa kwa wakati, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda hadhi ya taaluma, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini hauathiriki.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...