Na Byera Deus, Bukoba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia askari 13 wa taasisi mbalimbali za ulinzi na usimamizi wa rasilimali za misitu na wanyamapori kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu wanne waliokuwa wakisafirisha mkaa katika Kijiji cha Kanyamika, Kata ya Karambi, Tarafa ya Kimwani, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, tukio hilo lilitokea Oktoba 17, 2026, majira ya saa 10 jioni, katika eneo la Kanyamika, kando ya barabara kuu ya Muleba kuelekea Biharamulo, wakati askari hao walipokuwa doria katika Pori la Hifadhi ya Misitu ya Ruiga, wilayani Muleba.
Chatanda alisema askari hao walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili 02 JU 0354, mali ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wakiwa na askari wa wanyamapori na askari wengine waliokuwa kwenye doria hiyo.
Alieleza kuwa katika tukio hilo, watu waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa kutumia takribani pikipiki 10 wanadaiwa kukataa kukamatwa na kujaribu kuwanyang'anya askari silaha, hali iliyosababisha mapambano na matumizi ya silaha aina ya AK-47, ambapo watu wanne walipoteza maisha.
Watu waliotajwa kufariki dunia ni Osward Yuster, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Ngote; Pius Charles, miaka 40, mkazi wa Magata; Charles Michael, miaka 35, mkazi wa Ngote; na Edgar Elias Lukangula, miaka 44, mkazi wa Butembo, aliyefariki dunia alfajiri ya Oktoba 18, 2026, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanaoshikiliwa ni Mituni Haji (26), Faustin William Mboko (25), Kingmar Mewama (40), Fluomena Romani France (28), Erick David Muya (25), Yusuph Idd Kweya (26), Emmanuel Sheki Zabron (25), Yusto David (22), Josiah Msafiri Mahenge (26), Farouk Bashiru Mahamudu (24), Baraka Sadoki Kabulo (28), Regan Bwemelo Nikodem (24), Alanus Beyanga Chowe (35) na Andrew Charles Kwiyega (32), anayetajwa kuwa dereva wa TFS.
Aidha, tukio hilo lilisababisha uharibifu wa gari la Serikali aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya TFS, ambapo kioo cha mbele na vioo vya pembeni kwenye milango viliharibiwa.
Chatanda alisema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilipata na kukamata vitu mbalimbali vinavyohusishwa na tukio hilo, vikiwemo pikipiki 10, magunia 22 ya mkaa, mapanga matano, kofia ngumu mbili, makoti mawili, silaha tatu aina ya AK-47, maganda matano ya risasi za AK-47 pamoja na gari hilo la TFS.
Alisema watuhumiwa wote wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kubaini mazingira ya tukio hilo na kuchukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limeendelea kutoa wito kwa wananchi kutii sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi wanapokutana na mamlaka zilizopewa dhamana ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...