Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, wametaka maeneo maalumu ya kilimo na ufugaji kutengwa na kusimamiwa ipasavyo ili kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Nyongo ametoa agizo hilo kwa viongozi wa wilaya, akiwataka kuhakikisha maeneo ya malisho ya mifugo yanatengwa ili kupunguza migogoro inayojirudia kati ya makundi hayo.

Amesema tayari ametoa tamko la kutenga maeneo maalumu ya malisho, akisisitiza kuwa hataki kuona mauaji yanayotokana na migogoro hiyo.

“Nimeshatoa tamko la kutenga maeneo hayo kuondoa magomvi hayo na katika mkoa wangu sitaki kuona mauaji ya wakulima na wafugaji,” alisema Nyongo, akibainisha kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa.

Aidha, amewataka wakulima na wafugaji kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia kamati za usuluhishi kutatua changamoto zao kwa mujibu wa sheria.

Pia, amewataka wakulima na wafugaji kuzingatia taratibu zinazokubalika katika matumizi ya ardhi, huku akisisitiza umuhimu wa wafugaji kuepuka kuingiza mifugo katika mashamba ya watu na kuharibu mazao.

Kwa upande wake, Kikwete amewataka viongozi wa vijiji, Serikali na vyombo vinavyohusika kusimamia matumizi ya ardhi na kudhibiti uingizaji holela wa mifugo katika mashamba ya wakulima.

Amesema migogoro hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushindani wa matumizi ya ardhi, maji na malisho, pamoja na uhamaji wa wafugaji wanaotafuta rasilimali hizo.

Kutokana na hali hiyo, amependekeza kutengwa kwa maeneo maalumu ya kilimo na ufugaji, kusimamiwa kwa njia za kupitisha mifugo na kusajiliwa kwa wakulima na wafugaji ili kurahisisha usimamizi wa shughuli zao.

Kikwete pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha vikao vya ujirani mwema vitakavyowapa wakulima na wafugaji nafasi ya kujadili na kutatua changamoto zao kwa pamoja kabla hazijazua migogoro mikubwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema Serikali imekuwa ikifanya operesheni za kukabiliana na migogoro ya ardhi, ikiwemo inayohusisha wakulima na wafugaji.

Amesema jitihada hizo zinaambatana na kuhamasisha umoja, amani na kuheshimiana, kwa kuzingatia maeneo na shughuli za kiuchumi za kila kundi.

Kwa upande wake, mfugaji wa Chalinze, Seleman Hassan, ameishukuru Serikali kwa kutoa elimu kwa wafugaji, akisema wataendelea kushirikiana na wakulima ili kuondoa kero zinazojitokeza na kudumisha amani katika maeneo wanayoishi.

Migogoro ya wakulima na wafugaji imeendelea kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani, yakiwemo Chalinze, Bagamoyo, Rufiji, Kisarawe, Kibaha Vijijini na Kibiti.











Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...