Na Mwandishi Wetu, Mirerani
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeelezwa kuwa jumla ya gramu 274,634.32 za madini ya Tanzanite, zenye thamani ya Sh3.23 bilioni, zimezalishwa katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026.
Takwimu hizo zimetolewa na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Mirerani (RMO), George Kaseza, mbele ya kamati hiyo ilipotembelea maeneo ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite kwa lengo la kujifunza na kutathmini shughuli za uchimbaji, biashara na uongezaji thamani wa madini hayo.
Kaseza amesema uzalishaji huo ni wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, huku akieleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha usalama na usimamizi wa shughuli za uchimbaji ndani ya Ukuta wa Mirerani.
Amesema hatua hizo zinajumuisha ujenzi wa ukuta uliokamilika Aprili 2018, kuanzishwa kwa Soko la Madini la Mirerani mwaka 2021, pamoja na uwekaji wa kamera 310 za CCTV na taa 573 za usalama.
Aidha, amesema mwaka 2026 Serikali iliagiza kofia ngumu 12 zenye kamera kwa ajili ya wadhibiti wa shughuli za uchimbaji chini ya migodi.
Akizungumzia biashara ya Tanzanite, Kaseza amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, mnada wa wafanyabiashara wadogo uliofanyika Mei 15, 2026, ulihusisha uuzaji wa gramu 2,809.31 za madini hayo, zilizoripotiwa kuwa na thamani ya Sh271.270 bilioni.
Amesema mnada wa wafanyabiashara wakubwa uliofanyika Mei 21, 2026, uliwezesha kuuzwa kwa gramu 10,174.92 za Tanzanite, zenye thamani iliyoripotiwa kuwa Sh721.750 bilioni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgalu, amesema ziara hiyo imelenga kujifunza na kutathmini shughuli za uchimbaji, biashara na uongezaji thamani wa madini zinazofanyika ndani ya Ukuta wa Mirerani.
Akitoa maoni ya wadau wa sekta hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA), Elisha Mnyawi, ameiomba Serikali kuruhusu lango la kuingia na kutoka ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite kufanya kazi saa 24.
Mnyawi amesema kwa sasa, ifikapo saa 12 jioni, wachimbaji hawaruhusiwi kuingiza zana za kazi, hali ambayo amesema inahitaji kuangaliwa ili kurahisisha shughuli za uchimbaji.
Naye Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani, Samwel Rugemalila, ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua kuboresha sekta ya madini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Madini ndani ya Ukuta wa Mirerani, Magreth Nelson, ameishukuru Serikali kwa kurejesha minada ya madini, akisema hatua hiyo imewawezesha wafanyabiashara kuuza madini yao kwa uwazi na katika mazingira ya ushindani wa bei.
Hata hivyo, mjumbe wa chama cha wafanyabiashara wa madini, Victor Kunyara, ameiomba kamati hiyo kuangalia uwezekano wa kuweka kanuni zitakazowataka wachimbaji kutenga asilimia 10 ya uzalishaji wao na kuwauzia wafanyabiashara wa ndani.
Amesema hatua hiyo itasaidia wafanyabiashara kupata madini kwa ajili ya biashara zao na kuongeza uwezekano wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...