Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MKOA wa Pwani unalenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi hadi kufikia asilimia 50 kupitia kampeni ya Samia Legal Aid Awamu ya Pili, itakayotekelezwa kwa siku 10 katika halmashauri tisa za mkoa huo.

Ufunguzi rasmi wa kampeni hiyo unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2026, katika uwanja wa stendi ya zamani, Maili Moja, mjini Kibaha, huku utoaji wa huduma ukianza Oktoba 29 hadi Novemba 7, mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema kampeni hiyo itatoa fursa kwa wananchi kupata ushauri na huduma za msaada wa kisheria, kuwasilisha changamoto zao na kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria, yakiwemo ndoa na talaka, mirathi na wosia, ardhi pamoja na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.

Amesema wananchi wenye mashauri mahakamani au katika vyombo vingine vya utoaji haki pia watanufaika na huduma za uwakili zitakazotolewa bure na mawakili wa kujitegemea pamoja na mawakili wa serikali walioidhinishwa kutoa huduma hizo.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo itahusisha pia huduma za usajili wa matukio muhimu ya kibinadamu kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ikiwemo usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo.

Kwa mujibu wa Nyongo, kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha upatikanaji wa haki, hususan kwa makundi yenye uhitaji zaidi, yakiwemo wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Osborn Paisi, amesema awamu ya kwanza iliwafikia wananchi 200,000, sawa na asilimia 9 na kutoa huduma katika kata 10 na vijiji vitatu kila wilaya, huku awamu ya pili ikilenga kufikia kata 136 za Mkoa huo.


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...