Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesisitiza kuwa wananchi wenye bima ya afya wanapaswa kupata huduma bila vikwazo visivyo halali, huku akielekeza vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na huduma muhimu kwa wagonjwa.

Nyongo ametoa maelekezo hayo wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote uliofanyika Maili Moja, Kibaha, mkoani Pwani, akiwataka wakuu wa wilaya na watendaji wao kuimarisha uhamasishaji ili wananchi waelewe umuhimu wa bima hiyo, faida zake na utaratibu wa kujiunga.

Amesisitiza kuwa usajili unapaswa kuratibiwa katika vijiji, mitaa na kata zote, huku Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukitakiwa kuweka mawakala katika maeneo husika ili kurahisisha wananchi kujiunga na mpango huo.

Aidha, ameelekeza kufanyika kwa tathmini ya usajili baada ya siku 10 ili kubaini hatua iliyofikiwa na changamoto zinazohitaji kutatuliwa.

Ameagiza taarifa za utekelezaji kuwasilishwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa, huku wakuu wa wilaya wakitakiwa kusimamia zoezi hilo kwa karibu.

Nyongo pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia utekelezaji wa mpango huo unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Pwani, Tully Mwakyusa, amesema katika awamu ya kwanza, kaya 4,463 kati ya 6,212 zilizolengwa zimesajiliwa, sawa na asilimia 72 ya lengo lililowekwa.

Amesema awamu ya pili inalenga kusajili kaya 12,872 zenye jumla ya wanufaika 23,304, ikihusisha wananchi wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale wenye uwezo wa kuchangia gharama za bima.

Mwakyusa amesema kaya yenye watu wasiozidi sita itachangia Shilingi 150,000 kujiunga na mpango huo, huku Serikali ikianza tangu Februari 2026 kugharamia bima kwa makundi maalumu yenye uhitaji, yakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...