Jane Mwakyoma, Rukwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema thamani ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imeongezeka kutoka Sh. trilioni 7.4 mwaka 2021 hadi Sh. trilioni 16.96 kwa sasa, huku akiwataka watumishi wa umma kujiandaa mapema kwa maisha ya kustaafu.

Sangu ametoa kauli hiyo wakati wa kufungua semina ya watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu iliyofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya kifedha, kiafya, kifamilia na kiuchumi ili kuwawezesha wastaafu kuishi kwa utulivu na heshima baada ya kumaliza utumishi wao.

Amesema kustaafu ni hatua muhimu inayohitaji mipango ya kina, ikiwemo maandalizi ya makazi, afya ya mwili na akili, pamoja na kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowawezesha wastaafu kuendelea kujikimu baada ya ajira.

Kwa mujibu wa Sangu, semina hiyo inalenga kuwapa watumishi uelewa kuhusu mafao wanayostahili, nyaraka zinazohitajika katika mchakato wa malipo na namna bora ya kusimamia fedha watakazopokea baada ya kustaafu.

Aidha, amewataka watumishi kutumia mifumo ya kidijitali ya PSSSF kufuatilia taarifa za uanachama, michango na madai yao, huku akisisitiza umuhimu wa waajiri kuwasilisha michango kwa wakati ili kulinda haki za wanachama.

Akizungumzia ukuaji wa mfuko huo, Sangu amesema mwaka 2021, Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani, PSSSF ilikuwa na thamani ya Sh. trilioni 7.4 na deni la Sh. trilioni 4.6.

Amesema katika kipindi hicho, Sh. trilioni 4.2 zililipwa katika madeni hayo, hatua iliyochangia kuimarika kwa ukwasi wa mfuko na kuongezeka kwa thamani yake hadi Sh. trilioni 12.46 mwaka 2025, kabla ya kufikia Sh. trilioni 16.96 kwa sasa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali imeongeza kiwango cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka Sh. 100,000 hadi Sh. 250,000, hata pale pensheni inayotokana na mshahara wa mstaafu inapokuwa chini ya kiwango hicho.

Amesisitiza kuwa PSSSF inapaswa kuendelea kutoa huduma bora, za haraka, sahihi na zenye uwazi, kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia hifadhi ya jamii nchini.

Awali, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa PSSSF, Paul Kijazi, amesema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2018 kufuatia kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii iliyokuwepo wakati huo.

Amesema idadi ya wastaafu wanaopokea pensheni ya kila mwezi imeongezeka kutoka 115,390 wakati mfuko ulipoanzishwa hadi 183,228 kufikia Juni 2026. Aidha, tangu mwaka 2018, jumla ya wanachama 390,761 wamelipwa mafao yenye thamani ya Sh. trilioni 12.94.

Kijazi amesema PSSSF imeendelea kuboresha huduma zake kupitia kauli mbiu ya “Tunalipa Jana,” inayolenga kuonesha dhamira ya mfuko kulipa mafao kwa haraka baada ya wanachama kukamilisha taratibu zinazohitajika.

Ameongeza kuwa semina kwa watumishi wanaokaribia kustaafu ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha zao, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji. Katika kutekeleza hilo, taasisi za kibenki zimeshirikishwa kutoa elimu kuhusu usimamizi wa fedha na mipango ya maisha baada ya ajira.

Aidha, amesema matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano yamerahisisha upatikanaji wa huduma kupitia mifumo ya PSSSF Kiganjani na PSSSF Portal, inayowawezesha wanachama kufuatilia taarifa na mafao yao bila kulazimika kufika ofisini, hivyo kupunguza gharama za usafiri.

Amewataka pia wanachama kuwa waangalifu dhidi ya matapeli wanaojifanya watumishi wa mfuko huo kwa lengo la kuwaibia fedha.

Akihitimisha, Sangu amesisitiza kuwa kustaafu si mwisho wa kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya maisha inayohitaji mipango madhubuti, elimu ya kifedha na uelewa wa haki za hifadhi ya jamii ili mafao yanayopatikana yaweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...