Na Janeth Raphael -MichuziTv

Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi na utekelezaji wa Mradi wa Kuendeleza Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi, ikitoa maagizo matatu muhimu ikiwemo kukamilishwa kwa wakati kwa tafiti za mradi, ukusanyaji wa taarifa sahihi za utekelezaji pamoja na matumizi sahihi na utunzaji wa vitendea kazi vilivyotolewa.

 Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi magari, pikipiki na vifaa vya ugani kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Dkt. Bashiru ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma, ambapo amesema Ofisi ya Mradi inapaswa kuhakikisha tafiti zinazohitajika zinakamilishwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, sambamba na kuwepo kwa taarifa sahihi, kamili na zinazoaminika kuhusu utekelezaji wa shughuli za mradi. 

Amesema ukusanyaji wa taarifa kutoka Halmashauri na taasisi zinazoshiriki katika mradi huo unapaswa kukamilika, huku teknolojia mpya zikitumika kuhakiki maeneo ya utekelezaji na walengwa ili kuondoa uwezekano wa taarifa zisizo sahihi au zisizoweza kuthibitishwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Bashiru amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha vitendea kazi vilivyotolewa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kutunzwa ipasavyo ili viweze kudumu na kuendelea kuleta tija. 

Mradi huo umepokea pikipiki 23, ambapo 17 zimetolewa kwa Tanzania Bara na sita kwa Zanzibar, pamoja na magari sita, matatu kwa Tanzania Bara na matatu kwa Zanzibar, sambamba na vifaa mbalimbali vya ugani vitakavyosaidia shughuli za utekelezaji wa mradi.

Ameagiza kila chombo kilichotolewa kisajiliwe na kukabidhiwa kwa mtumiaji anayestahili, huku kumbukumbu sahihi za matumizi, matengenezo na ukarabati zikiwekwa. 

Aidha, amesisitiza kuwa magari hayo yanapaswa kutumika kwa shughuli za mradi pekee, kwa kuzingatia uzito wa mizigo, hali ya barabara na matengenezo ya wakati, wakati pikipiki zikitumika katika ufuatiliaji wa shughuli za mradi kulingana na maeneo yaliyopangwa. Ameonya kuwa atakayekiuka maelekezo hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame, amesema mifugo ni sehemu ya maisha na utajiri wa wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta hiyo. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Suleiman Makame amewashukuru viongozi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo, akisema umevuka hatua ya awali ya dhana na sasa umefikia hatua ya utekelezaji unaohitaji usimamizi madhubuti.

Suleiman Makame amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa viongozi, watendaji na wadau wote, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa. 

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kuimarika, kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na hatimaye kuleta manufaa yanayotarajiwa kwa wananchi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...