Na Janeth Raphael - MichuziTv - Bungeni

Serikali imeimarisha mikakati ya kusimamia na kutathmini utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo nchini kupitia mfumo wa kielektroniki wa e-Delivery, unaolenga kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo yanayochochea kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hatua hiyo pia inalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya umma, huku Bunge na wananchi wakipata fursa ya kufuatilia maendeleo ya mipango ya Serikali na kupima matokeo yake kupitia dashibodi za mfumo huo.

Akijibu swali la Mbunge wa Magomeni, Imamu Mtumwa Vuai, leo Oktoba 27, 2026, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amesema mfumo huo umeundwa kuunganisha mipango ya maendeleo ya muda mrefu, wa kati na mfupi ili kuhakikisha utekelezaji wake unaendana na vipaumbele vya Taifa.

Amesema mfumo wa e-Delivery unahusisha Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa mwaka 2026/27 hadi 2050/51, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), mipango ya kisekta na kikanda, pamoja na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya mwaka 2030 na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063.

Kwa mujibu wa Dkt. Chaya, kuunganisha mipango hiyo kutarahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wake na kuwezesha Serikali kutathmini mchango wa miradi mbalimbali katika kufikia malengo ya maendeleo ya nchi.

Katika kuhakikisha mfumo huo unatumika ipasavyo, amesema Serikali imetoa mafunzo kwa watumishi takribani 940 kutoka wizara, taasisi za umma, mikoa na halmashauri kuhusu matumizi yake.

Aidha, amezitaka taasisi zote za umma kutumia e-Delivery katika hatua zote za usimamizi wa miradi, kuanzia uibuaji, uandaaji na uidhinishaji hadi ufuatiliaji na tathmini. Pia amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati na kusajili miradi yote ya maendeleo inayoendelea katika mfumo huo.

Hatua hiyo inatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hali ya miradi, hatua iliyofikiwa na matokeo yanayopatikana, huku ikiwezesha kupima kwa ufanisi zaidi mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...