Na Janeth Raphael - MichuziTv Bungeni

Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Moses Nnauye, amesema Tanzania imeweka historia kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa umoja huo mwaka 1889.

Nape ameeleza kuwa mafanikio hayo ni hatua muhimu kwa Tanzania katika kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kimataifa, hususan katika kuendeleza ushirikiano wa mabunge na kukuza misingi ya utawala bora duniani.

Akisoma Azimio la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Nape amesema mkutano huo uliofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, umeonesha uwezo wa Tanzania wa kuandaa na kuratibu mikutano mikubwa ya kimataifa.

Amesema mkutano huo uliofanyika chini ya kauli mbiu ya “Kuimarisha Utawala Bora na Kuziwezesha Jamii” umeipa Tanzania fursa ya kuonesha utayari wake katika kushiriki mijadala ya kimataifa inayolenga kuimarisha utawala bora na kuwawezesha wananchi.

Aidha, mafanikio ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha nafasi ya mabunge kama taasisi muhimu katika kusimamia uwajibikaji, uwakilishi wa wananchi na demokrasia.

Nape ameyasema hayo leo, Oktoba 27, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha azimio hilo katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Tano wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Azimio hilo limelenga kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, ambao umeweka alama muhimu katika historia ya ushiriki wa nchi katika shughuli za Umoja wa Mabunge Duniani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...