Farida Mangube, Morogoro 

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewataka wakufunzi kubuni mbinu mpya za ufundishaji zinazoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hususani matumizi ya Akili Unde (AI), ili kuimarisha utoaji wa elimu na kuhakikisha wanafunzi hawaachwi nyuma katika ulimwengu wa kidijitali.

Dkt. Shein amesema maendeleo ya teknolojia yanabadilisha kwa kasi namna taarifa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kusambazwa katika jamii, hivyo ni muhimu kwa wakufunzi kuendana na mabadiliko hayo huku wakizingatia maadili na wajibu wa binadamu katika kufanya maamuzi yenye busara.

Amesema akili unde ina uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa na matukio kwa haraka, jambo linaloonesha umuhimu wa taasisi za elimu ya juu kujiandaa na mabadiliko hayo ili zisibaki nyuma.

Amesisitiza kuwa pamoja na teknolojia kuwa na uwezo wa kutafuta taarifa na kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali, haiwezi kuchukua nafasi ya binadamu katika kufanya maamuzi yanayozingatia busara, maadili na uwajibikaji.

Amesema ni muhimu kwa wakufunzi kutafuta mbinu mpya za kutumia taaluma zao katika kufundisha wanafunzi, huku wakitoa tahadhari kuhusu misingi ya matumizi sahihi ya teknolojia hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Baraza limefanya kazi kubwa kuimarisha utawala bora na kuhakikisha rasilimali za chuo zinatumika kwa kuzingatia misingi ya usimamizi wa fedha za umma.

Balozi Mero amesema usimamizi bora wa rasilimali ni muhimu katika kuhakikisha chuo kinafanya kazi kwa ufanisi na kutekeleza majukumu yake ya kutoa elimu ya juu kwa kuzingatia uwajibikaji.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amesema chuo hicho kinaendelea kuunganisha elimu ya juu na vipaumbele vya maendeleo ya taifa kupitia ushiriki wake katika majukwaa ya kimataifa.

Amesema ushiriki huo ni muhimu katika kuimarisha mchango wa elimu ya juu katika maendeleo ya taifa na kupanua ushirikiano wa chuo na wadau mbalimbali wa kimataifa.

kwa upande wak Mlau Profesa Elizabeth Lulu Genda  amewapongeza wahitimu na kuwataka kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri, nidhamu na uvumilivu.

Amesema maisha yana milima na mabonde, hivyo wahitimu wanapaswa kuwa jasiri na watiifu katika safari yao ya maisha ili waweze kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wanapotekeleza majukumu yao katika jamii.

Ameongeza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa na msimamo, kujituma na kuzingatia maadili katika kutafuta mafanikio, wakitambua kuwa changamoto ni sehemu ya safari ya maisha.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...