Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO Dkt.Venance Mwase akizungumza na wahariri kuhusiana na mafanikio na Mikakati Jijini Dar es Salaam.

Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Alex Malanga akizungumza kuhusiana na Ofisi hiyo ilivyojipanga katika Taasisi zilizochini ya Msajili kutoa taarifa za maandeleo
Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile akizungumza kuhusiana na umuhimu wa taarifa kwa wananchi kuhusiana na rasilimali zao zikiwemo Madini,jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya matukio katika picha Katika mkutano uliohusisha wahariri na STAMICO
Picha ya pamoja.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake kutoka takribani Sh bilioni 1.3 hadi Sh bilioni 149.8, huku likiendelea kuweka mikakati ya kuimarisha miradi ya uchimbaji, kuongeza uzalishaji na kupanua huduma kwa wachimbaji wadogo nchini.

Mikakati hiyo inahusisha kuongeza mitambo ya uchorongaji, kuendeleza viwanda vya uchakataji wa madini, kuimarisha tafiti za kijiolojia na kuwaunganisha wachimbaji wadogo na taasisi za fedha ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika kikao kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Dkt. Venance Mwase, amesema shirika hilo limeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha utendaji wake, kuongeza uzalishaji na kusimamia masilahi ya wachimbaji wadogo.

Amesema katika kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo, STAMICO imebaini changamoto zinazowakabili wachimbaji, zikiwemo ukosefu wa taarifa za kijiolojia, mitaji, elimu ya uchimbaji na matumizi ya teknolojia zinazoweza kuongeza tija katika uzalishaji.

Ameeleza kuwa hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuimarisha tafiti za kijiolojia, kuongeza mitambo ya uchimbaji na uchorongaji pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia katika shughuli zao.

Aidha, shirika hilo linaweka mikakati ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo na viwanda vya uchakataji wa madini ili kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

MIRADI YA UCHIMBAJI NA VIWANDA
Katika kuendeleza shughuli za uzalishaji, STAMICO imeendelea kusimamia miradi yake ya uchimbaji kwa kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi na kuboresha matumizi ya rasilimali zilizopo.

Dkt. Mwase amesema miongoni mwa miradi inayosimamiwa na shirika hilo ni mradi wa Kiwila, ambako juhudi zinaendelea katika kukarabati majengo na kuboresha miundombinu inayohitajika kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.

Amesema pia shirika lina mpango wa kuimarisha huduma za uchorongaji kwa kuongeza mitambo ili kupanua wigo wa huduma kwa wateja wanaojihusisha na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.

Katika eneo la viwanda, STAMICO ina mipango ya kuendeleza shughuli za uchakataji wa madini katika maeneo ya Tabora, Singida na Kiwila, pamoja na kuwa na mpango wa kuweka mtambo wa kutengeneza kokoto jijini Dodoma.

Hatua hizo zinalenga kuongeza thamani ya madini na malighafi zinazozalishwa nchini kabla ya kuuzwa sokoni, huku zikifungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira.

WACHIMBAJI WADOGO KUNUFAIKA
STAMICO imeweka msisitizo katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata huduma na teknolojia zitakazoboresha shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kukuza mapato.

Kupitia mikakati hiyo, wachimbaji wadogo wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa taarifa za kijiolojia, elimu ya uchimbaji, teknolojia bora na fursa za kupata mitaji kupitia ushirikiano na taasisi za fedha.

Shirika hilo pia lina mpango wa kuwaunganisha wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi na viwanda vinavyoweza kutumia malighafi wanazozalisha.

Kwa mujibu wa mikakati hiyo, hatua hiyo inalenga kupanua soko la bidhaa zao, kuimarisha mnyororo wa thamani na kuongeza mchango wa shughuli za uchimbaji katika uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

MAGEUZI YAIMARISHA MAPATO
Katika historia yake, STAMICO imepitia changamoto mbalimbali zilizoathiri shughuli zake na maendeleo ya baadhi ya miradi, hali iliyohitaji bodi na menejimenti kuweka mikakati ya kuboresha utendaji na kuimarisha uwezo wa shirika kujiendesha kifedha.

Mwaka 2020, Serikali iliendelea kusisitiza mageuzi ya kiutendaji kupitia falsafa ya 4R ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayohusisha maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya.

Katika kipindi hicho, shirika liliweka mikakati ya kuboresha usimamizi wa miradi na watumishi, kuongeza ufanisi wa shughuli zake na kuimarisha uwezo wa kujiendesha kifedha.

STAMICO inaendelea kulenga kuimarisha shughuli zake za kibiashara, kuongeza mchango wake katika maendeleo ya sekta ya madini na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata fursa zaidi za kushiriki katika shughuli za uzalishaji na uchakataji wa madini nchini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...