Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na taasisi za uhifadhi wa mazingira, limeadhimisha kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kupanda miti ya kumbukumbu katika taasisi za umma, ikiwemo shule.
Zoezi hilo limefanyika jana, Oktoba 27, 2026, katika Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuenzi urithi na mchango wake katika ujenzi wa taifa na uhifadhi wa mazingira.
Akiongoza zoezi hilo, mtoto wa Baba wa Taifa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, alisema taifa litaendelea kumkumbuka Mwalimu Nyerere kwa uzalendo wake, uadilifu na moyo wa kulitumikia taifa, sambamba na misingi ya mshikamano aliyoiacha ambayo imeendelea kuwa nguzo ya umoja na amani nchini.
Makongoro aliwataka vijana wa Kitanzania kuzingatia uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa, huku akiwahimiza kuenzi misingi ya Mwalimu Nyerere kwa kutunza mazingira, kulinda maeneo yaliyohifadhiwa na vyanzo vya maji, pamoja na kupanda miti katika makazi yao kwa ajili ya kupata vivuli na matunda.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Emmanuel Moirana, alisema shirika hilo litaendelea kuenzi mchango wa Hayati Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa mwanzilishi wa TANAPA.
Alisema maono ya Baba wa Taifa yameendelea kuwa dira ya uhifadhi endelevu nchini, huku matokeo yake yakionekana kupitia maendeleo ya sekta ya utalii na ongezeko la watalii wanaotembelea vivutio vya Tanzania.
Moirana aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere atakumbukwa pia kwa kusisitiza umuhimu wa amani, uzalendo, mshikamano na kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao.
Alisisitiza kuwa rasilimali za taifa zinapaswa kusimamiwa kwa manufaa ya Watanzania wote, akihimiza wananchi kuendeleza misingi hiyo kwa kulinda mazingira na kuhifadhi urithi wa taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...