Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TANZANIA imetoa wito kwa nchi wanachama zinazopakana na Ziwa Tanganyika kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya kikanda ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na shinikizo la matumizi ya rasilimali zinazotishia mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Dk. Richard Muyungi, leo Oktoba 25, 2026, wakati akifungua Mkutano wa 15 wa Kawaida wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaofanyika Dar es Salaam.
Dk. Muyungi amesema kulinda ziwa hilo kunahitaji ushirikiano wa kikanda, ufuatiliaji madhubuti wa mazingira na uwajibikaji ili kuhakikisha maazimio yanayofikiwa yanatekelezwa kwa vitendo.
Amesema mkutano huo unajadili mpango kazi na bajeti ya mamlaka hiyo kwa mwaka 2026 pamoja na utekelezaji wa maazimio ya mawaziri yaliyopitishwa mjini Livingstone, Zambia.
Ameonya kuwa kuharibika kwa mazingira ya ziwa hilo kunatishia maisha na kipato cha mamilioni ya watu wanaotegemea rasilimali zake, hivyo Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia zinapaswa kuratibu mikakati ya kulinda ziwa hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Dk. Emma Liwenga, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuboresha Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa mwaka 2012 na kuandaa ripoti ya kina ya bonde la ziwa hilo kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF).
Amesema mipango mingine ni pamoja na tathmini ya hali ya samaki katika ziwa lote inayoungwa mkono na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), pamoja na miradi ya uhifadhi wa bayoanuwai na usalama wa maji.
Mwenyekiti wa mkutano huo, Richard Mlungu, amesema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu kwa nchi wanachama kutokana na mchango wake katika upatikanaji wa maji, uvuvi, bayoanuwai na shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, amesema ziwa hilo linakabiliwa na changamoto zinazoongezeka, zikiwemo uvuvi usio endelevu, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa makazi ya viumbe hai, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu.
Amesema mkutano huo pia unajadili ripoti ya mwaka ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), mpango kazi na bajeti ya mwaka 2027, huku akizitaka nchi wanachama kuongeza ushirikiano na rasilimali za kifedha kwa ajili ya kulinda ziwa hilo.
Naye Mkurugenzi wa Mazingira na Mjumbe wa Kamati, Kemilembe Mutasa, amesema Ziwa Tanganyika si mpaka wa kijiografia unaotenganisha nchi wanachama, bali ni rasilimali inayozileta pamoja kutokana na mchango wake katika maisha ya wananchi, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema maamuzi na ushauri wa Kamati ya Usimamizi kwa Baraza la Mawaziri la mamlaka hiyo ni muhimu katika kuhakikisha linatekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kusimamia rasilimali za ziwa hilo kwa uendelevu.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...