Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameitaka Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuhakikisha miradi ya kuboresha miundombinu ya utalii inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Amesema uboreshaji wa miundombinu katika vivutio vya utalii vya Maporomoko ya Maji ya Endoro na Mapango ya Tembo ni sehemu ya jitihada za kufanikisha azma ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kufikisha idadi ya watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya miradi hiyo, ambapo alieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake, akisisitiza kuwa fedha za miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (TDL) zinapatikana na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wake.
Amesema hadi sasa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imetengewa Sh bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa barabara, huku akibainisha kuwa wakandarasi wanaendelea kulipwa kulingana na hatua za utekelezaji wa kazi.
Aidha, amesema Sh bilioni 1.67 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha vivutio vya utalii vya Endoro na Ngoitoktok vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro. Miradi hiyo imefikia asilimia 68 ya utekelezaji na inatarajiwa kukamilika Desemba 2026.
Msimamizi wa miradi hiyo, SACC Mariam Kobelo, amesema mradi wa Endoro unahusisha ujenzi wa majengo ya ofisi, geti, njia za kutembelea kwa miguu zenye urefu wa mita 2,200, njia za mbao (boardwalk), alama za maelekezo, vyoo pamoja na maeneo ya wageni kupumzikia.
Ameongeza kuwa mradi wa Ngoitoktok unalenga kuboresha mazingira ya eneo la mapumziko ya wageni kwa kuongeza miundombinu itakayowawezesha watalii kukaa na kupumzika kwa urahisi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, Abdul-Razaq Badru, amesema ujenzi wa barabara ya tabaka gumu kutoka Loduare hadi Geti la Seneto, yenye urefu wa kilomita 29.5, unaendelea vizuri.
Amesema mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kwa gharama ya Sh bilioni 80.36 umefikia asilimia nane ya utekelezaji, huku juhudi zikiendelea kuimarisha usimamizi na kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.



.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...