-Mpango wa TASAF wamuwezesha kujenga nyumba bora,kuanzisha bishara kujipatia kipato


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

SERIKALI ya Tanzania mwaka 2002 ilianza kutekeleza mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii)TASAF)ikiwa ni moja ya mbinu za kutokomeza umasikini.

Kama lilivyolengo la kuanzishwa kwa mpango huo mamilioni ya Watanzania hasa kutoka Kaya maskini wamebadilisha maisha yao kutoka hali duni ya kutokuwa na uhakika wa kula wala pakulala.

Kupitia mpango huo wa TASAF kumekuwa na shuhuda nyingi kutoka kwa wanufaika wa mfuko huo na miongoni mwa wanufaika hao ni Mkazi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Bi.Graciana Petro ambaye anaishukuru Serikali kupitia TASAF ameweza kujikwamua kiuchumi.

Amejenga nyumba bora, tofauti na hali ngumu ya maisha aliyokuwa akiishi nayo kabla ya kunufaika na mpango huo.Ana uhakika wa milo mitatu huku maziwa mtindi yakiwa pembeni yake.TASAF wamebadilisha maisha yake,umasikini wa kipato kwake imebakia historia.

Graciana ambaye ni Mjane amesema kabla ya kujiunga na mpango huo, maisha yake yalikuwa magumu, huku akihangaika kutafuta mahitaji ya msingi kwa ajili yake na familia yake. Hali hiyo ilimfanya ashindwe kuboresha makazi yake kutokana na ukosefu wa kipato cha uhakika.Hivyo alikuwa akikaa kwenye nyumba ya udongo iliyoezekwa kwa nyasi.


Amesema kuanza kunufaika na fedha za TASAF kumekuwa hatua muhimu katika maisha yake, kwani kumemwezesha kuanzisha shughuli za kiuchumi na kutumia mapato anayopata kuboresha makazi yake pamoja na kuongeza uwezo wa kumudu mahitaji ya kila siku.

“Awali nilikuwa na hali ngumu sana ya maisha, lakini baada ya kujiunga na mpango huu nimeweza kujenga nyumba hii mnayoiona, ambayo ni bora zaidi kuliko makazi niliyokuwa nayo hapo awali,” amesema mjane huyo.

Ameeleza pamoja na kujenga nyumba hiyo, fedha alizopata kupitia mpango huo zimemwezesha kuanzisha biashara ndogo ya kuuza dagaa, nyanya, mafuta ya kupikia, vitunguu na bidhaa nyingine zinazohitajika na wananchi katika maisha ya kila siku.

Amesema biashara hiyo imekuwa chanzo muhimu cha kipato kinachomsaidia kununua chakula na mahitaji mengine ya nyumbani, huku akitumia faida anayopata kuendeleza biashara na kuimarisha hali yake ya kiuchumi.

Aidha, mjane huyo amepiga hatua nyingine kwa kununua mifugo, ambapo kwa sasa ana ng’ombe wanne na mbuzi wanne, jambo linalompa matumaini ya kuendelea kuboresha maisha yake na kujenga msingi wa maendeleo ya baadaye.

Amesema mafanikio hayo yamebadili hali yake ya maisha kwa kiasi kikubwa, kwani sasa ana makazi bora, shughuli za kujipatia kipato na mali zinazoweza kumsaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi.

Wakati wa kuadhimisha Siku ya Kutokomeza Umasikini Duniani ambayo hufanyika kila Oktoba 17 ,Mjane huyo ametumia siku hiyo kuelezea hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia TASAF kumtoa katika lindi la umasikini yeye na mamilioni ya Watanzania ambao huenda bila ya TASAF leo wangekuwa hawajui hatma ya maisha yao.
Mjane huyo amesema mbali ya kulala katika nyumba nzuri, kufuga na kufanya biashara ya kuuza genge kwa sasa hata watoto na wajuu zake wana uhakika wa elimu iliyobora na yenye uhakika na yote hayo yamefanikiwa kwasababu kuna mpango wa kusaidia kaya masikini kupitia TASAF.

Akizungumzia mabadiliko yanayopatikana kwa wanufaika wa mpango huo, Ofisa Mratibu wa TASAF Wilaya ya Misungwi, Gloria Bunambi, amesema mpango huo umechangia kuboresha maisha ya wananchi wenye hali duni za kiuchumi kwa kuwawezesha kukidhi mahitaji ya msingi na kupiga hatua katika shughuli zao za maendeleo binafsi.

Amesema kabla ya kunufaika na TASAF, baadhi ya kaya zilikuwa zikikabiliwa na changamoto za kupata hata mahitaji madogo kama chumvi, sabuni na viberiti, lakini kwa sasa baadhi yao wameimarika na wanaweza kujipangia malengo ya maendeleo kulingana na uwezo wao.

Amesema mabadiliko hayo yanaonekana pia kwa wanawake wanaojishughulisha na biashara katika masoko ya vijijini, kilimo, uuzaji wa mazao na shughuli nyingine zinazowawezesha kupata kipato na kuboresha maisha ya familia zao.

Ameongeza kuimarika kwa kipato cha kaya kumechangia kuboresha upatikanaji wa chakula, mavazi na mahitaji ya watoto, huku baadhi ya familia zikipata fursa ya kupanga namna ya kugharamia elimu ya watoto wao na mahitaji mengine muhimu.

Ameongeza mafanikio yanayoonekana kwa wanufaika yanaonesha umuhimu wa kuwawezesha wananchi wenye hali duni za maisha kupata fursa za kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha endelevu, akitoa shukrani kwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mpango huo.

Kwa mjane huyo, nyumba bora aliyoijenga ni ishara ya mabadiliko aliyoyapata kupitia TASAF, huku biashara na mifugo aliyonayo vikiendelea kuwa msingi wa matumaini yake ya kuimarisha kipato na kuishi maisha bora zaidi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...