-Asema wingi wa mavuno ulete maisha bora kwa wakulima

 WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mafanikio ya mageuzi ya kilimo yanapaswa kupimwa kwa ongezeko la kipato na ustawi wa wakulima na kuangalia zaidi suala la masoko ya uhakika, bei zenye tija na miundombinu ya kuhifadhi na kuchakata mazao.

“Kwa familia za wakulima, kupata mavuno mengi pekee hakumaanishi kwamba wamefanikiwa kiuchumi. Mavuno mazuri yanapaswa kuleta maisha bora kwa mkulima,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Oktoba 21, 2026) wakati akizungumza na vijana 75 kutoka mataifa mbalimbali wanaochipukia katika kilimo kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, Marekani.

 Akielezea kuhusu kaulimbiu yao, Waziri Mkuu alisema: “Kaulimbiu yenu isemayo ‘Wakati Wakulima Wanafanikiwa, Afrika Inastawi,’ inatukumbusha kwamba ni lazima tupime mageuzi ya kilimo kwa kuangalia mabadiliko yanayotokea kwenye maisha ya wakulima. Uzalishaji mkubwa ni muhimu. Lakini muhimu ni mapato yanayopatikana, usalama unaopatikana na fursa zinazojitokeza kwa familia.”

Dkt. Mwigulu ambaye anahudhuria mkutano kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema wakulima wanaweza kuongeza uzalishaji bila kuona manufaa yanayotarajiwa kutokana na gharama kubwa za usafirishaji, uhaba wa maghala na bei zisizofidia gharama za uzalishaji.

Dkt. Mwigulu alisema changamoto hizo zinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja ili kilimo kiwe biashara yenye manufaa na inayovutia vijana. Alisema kuwa Tanzania inaendelea kuwawezesha vijana kupata ardhi, kuwaunganisha na taasisi za fedha na kupanua matumizi ya teknolojia na mashine za kisasa za kilimo.

Alisema Serikali inaongeza uwekezaji katika miradi ya umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu bora, utafiti, huduma za ugani, maghala na miundombinu ya kuchakata mazao.

 Aidha, Waziri Mkuu amehimiza kuongeza uzalishaji wa ndani wa mbolea, mbegu bora na mafuta ya kula ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Amesema changamoto za hali ya uchumi duniani zimeonesha umuhimu wa kuimarisha uwezo wa ndani wa kuzalisha bidhaa muhimu kwa kilimo na chakula. 

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na vijana hao, Rais wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA), Alice Ruhweza aliipongeza Tanzania kwa hatua inazochukua katika kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya mashine za kilimo na kuwawezesha vijana. Pia, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri katika kuendeleza programu ya Jenga Kesho Bora (BBT).

 Alisema AGRA, kwa kushirikiana na Taasisi ya Mastercard (Mastercard Foundation), inaendesha programu ya kuwawezesha vijana katika kilimo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 350 katika nchi zinazoshiriki, ikiwemo Tanzania. Alisema kuwa utekelezaji wake nchini unaendana na BBT ili kuimarisha juhudi zilizopo badala ya kuanzisha programu zinazojirudia.

 Bi. Ruhweza alisema kwamba uzoefu wa Tanzania unaweza kutumika katika nchi nyingine za Afrika ili kuwainua kwenye kilimo.

Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Balozi wa Tanzania Washington, Dkt. Elsie Kanza na watendaji wengine wa Serikali.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...