NA DENIS MLOWE, IRINGA

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewaelekeza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wa serikali za mitaa kusimamia kwa vitendo usajili wa wananchi katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisisitiza kuwa idadi ya walioandikishwa na ubora wa huduma wanazopata vitakuwa miongoni mwa vigezo vya kupima utendaji wao wa kazi.

Akizungumza katika viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa, wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango huo, James alisema zoezi hilo halipaswi kuishia kwenye takwimu za usajili pekee, bali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa wakati na bila kukabiliwa na vikwazo visivyo vya lazima.

Alisema serikali inalenga kujenga mfumo utakaowezesha wananchi kupata matibabu bila familia kulazimika kuuza mali, kukopa au kuchelewesha matibabu kutokana na gharama kubwa kwani bima ya afya ni njia ya kulinda kipato cha kaya, nguvu kazi ya taifa na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Katika kusisitiza uwajibikaji Kheri James alisema atafuatilia utekelezaji wa mpango huo kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji, vitongoji, mitaa na kata na kuwaielekeza wakurugenzi na wakuu wa wilaya kukutana na watendaji wa maeneo yao kabla ya Oktoba 30, 2026, ili kuweka mikakati ya uhamasishaji na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati.

James alisema ofisi yake itaratibu ufuatiliaji wa usajili, utambuzi wa kaya zinazostahili kulipiwa na serikali, utayari wa vituo vya kutolea huduma, upatikanaji wa dawa na namna malalamiko ya wananchi yanavyoshughulikiwa. Alionya kuwa hataridhika na taarifa za watu kujiunga na bima ikiwa bado wanashindwa kupata huduma wanazostahili.

Akifafanua gharama za kujiunga na mpango huo, alisema kaya itatakiwa kulipa Sh150,000 kwa mwaka kwa kifurushi kinachojumuisha watu wasiozidi sita ambapo utaratibu huo unalenga kuipa familia uhakika wa kupata huduma za afya katika kipindi cha miezi 12, huku akiwahimiza wananchi kujiunga mapema badala ya kusubiri hadi wanapougua.

Alitoa mfano wa wafanyabiashara, waendesha bodaboda na bajaji, akisema makundi hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ajali hivyo kuwa na bima kutawasaidia kupata huduma katika vituo vinavyohusika wanapokuwa safarini au wanapokumbwa na matatizo ya kiafya nje ya maeneo wanayoishi, kwa kuzingatia masharti ya kifurushi walichojiunga nacho.

Aidha, alisema kaya maskini zitakazotambuliwa kuwa na uhitaji zitazingatiwa katika utaratibu wa kusaidiwa na serikali kupitia mifumo iliyowekwa, ikiwemo TASAF.

Alizitaka mamlaka za vijiji kushiriki katika utambuzi wa kaya hizo ili wananchi wanaostahili msaada wasiachwe nyuma katika utekelezaji wa mpango huo.

Kwa upande wa watoa huduma za afya, James alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha dawa zinapatikana, watumishi wanakuwepo na mifumo ya kuhakiki wanachama inafanya kazi ipasavyo na wananchi wanapata huduma wanazostahili bila kutozwa malipo ambayo hayajaidhinishwa katika vifurushi vyao, huku malalamiko yakipokelewa, kushughulikiwa na kutolewa mrejesho kwa wahusika.

Alionya kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kunyimwa huduma za dharura kwa sababu ya mabishano ya malipo au uhakiki wa bima na kusema kuwa kuwa uhai wa mgonjwa unapaswa kupewa kipaumbele, huku taratibu nyingine zikifuatwa baada ya hali ya mgonjwa kushughulikiwa.

Katika hatua nyingine, aliwataka viongozi wa dini, vikundi vya wakulima, wafanyabiashara, waajiri, taasisi binafsi na mashirika ya kijamii kushirikiana na serikali kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya.

Alisema wananchi wanapaswa kufahamu haki zao, wajibu wao, huduma zinazopatikana kwenye vifurushi vyao na njia rasmi za kuwasilisha malalamiko wanapokutana na changamoto.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yatapimwa kwa matokeo halisi katika maisha ya wananchi, yakiwemo upatikanaji wa huduma kwa wakati, ubora wa matibabu na kupungua kwa vikwazo vya kifedha vinavyoikabili familia inapokumbwa na ugonjwa.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...