Na George Maziku, Geita
BALOZI wa amani kutoka Shirikisho la Vyama vya wachimbaji wadogo wa madini nchini (FEMATA), Mess Chengula amewashauri vijana kubadilika na kuanza kuziona fursa za maisha na kuzitumia, badala ya kutumia muda mwingi kulalamikia serikali.
Mess ametoa ushauri huo jana mjini Masumbwe, wilayani Mbogwe, mkoani humo wakati akihojiwa na vyombo vya habari kuhusu fursa za kazi kwa vijana katika sekta ya madini ambamo yeye amekuwa akifanya kazi na kupata mafanikio makubwa.
"Mimi kama balozi wa amani nchini nawashauri vijana wenzangu kubadili mitazamo, wasitumie muda wao mwingi kulalamikia serikali kwamba haiwapi kazi. Wazione fursa zilizopo na kuzitumia kutengeneza maisha yao. Kwa mfano huku migodini tunakofanya kazi kuna fursa nyingi mno za kazi ambazo mtaji wake ni nguvu zako tu, hauhitaji mkopo wa mamilioni ya fedha ila unahitaji afya njema tu, hata mimi na vijana wenzangu tuliofanikiwa hatukuwa na mtaji wa fedha bali nguvu pekee", alibainisha Balozi Mess.
Aliongeza, "Hii serikali ya awamu ya sitta chini ya mama yetu mpendwa Rais Samia Suluhu Hassan inatupenda sana vijana wa kitanzania na inataka tufanikiwe kwa kuondokana na umaskini, ndio maana katika sekta hii ya madini serikali imekuja na mpango mahususi wa kutenga maeneo ambayo yatagawiwa kwa vijana wa kitanzania", alifafanua Balozi Mess.
"Lakini pia serikali imetuundia wizara kamili ya vijana ambayo kazi yake kubwa ni kutatua matatizo yetu, hususani matatizo ya ajira", alisisitiza Balozi Mess.
Mchimbaji huyo kijana ambaye amewekeza katika migodi mbalimbali ya wachimbaji wadogo nchini na kufanikiwa kujikusanyia utajiri mkubwa, alisema kuwa ameanza kuwakusanya vijana na kuwasaidia kupata fursa ya uchimbaji katika migodi mbalimbali nchini ukiwemo mgodi mpya wa dhahabu unaopatikana katika kijiji cha Lugunga, wilayani Mbogwe.
"Hivi karibuni nilialikwa kwenye kongamano mjini Mwanza, na baada ya kongamano lile niliwaambia vijana waangazie fursa za maisha migodini, na nilijitolea kuwatembeza katika migodi kadhaa kwa gharama zangu ili wajionee fursa na wazitumie kubadili maisha yao, nashukuru kuwaona baadhi yao wameanza kazi za uchimbaji", alihitimisha Balozi Mess.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...