Na Seif Mangwangi, Michuzi TV
WAKALA wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) umesema umeweka mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa maafisa ugani nchini kwa lengo la kuhakikisha wanawajibika kwa wakulima wanaowahudumia na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Aidha wakala huo umewataka wazalishaji wa mbegu kuiga mfano wa kampuni ya Bayer kwa kuzalisha mbegu bora na zenye tija Kwa wakulima kwa kuwa hakuna mbadala mwingine wa mbegu zaidi ya hizo za kisasa ambazo zimekuwa zikizalisha mazao mengi tofauti na mbegu za kienyeji.
Akizungumza na wakulima wa kata ya King'ori Halmashaurinya Meru Wilayani Arumeru kwenye ziara ya kutembelea wakulima iliyoandaliwa na kampuni ya mbegu ya Bayer, Mtendaji Mkuu wa NAESA, Dkt. Wilhelm Leonard Mafuru, amesema mfumo huo utaunganisha maafisa ugani na wakulima katika kata na vijiji wanavyohudumia huku ukirahisisha ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa na matokeo yake kwa wakulima.
Amesema NAESA imeanzishwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali, Sura ya 245, na kutangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Toleo Na. 156 la Juni 26, 2026, ikiwa na jukumu la kuratibu na kusimamia huduma za ugani nchini.
Dkt. Mafuru amesema wakala huo unalenga kuhakikisha wakulima wanapata huduma bora za ugani kutoka kwa maafisa wa sekta ya umma na binafsi, ili kuwawezesha kuongeza tija na uzalishaji kupitia matumizi ya maarifa na teknolojia za kisasa.
Amesema moja ya majukumu makuu ya NAESA ni kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa na taasisi za utafiti zinafikishwa kwa wakulima kwa wakati, ili zitumike katika kuboresha uzalishaji na kuendeleza kilimo kinachozingatia kanuni bora.
Ameongeza kuwa wakala huo utahakikisha wakulima wanapata elimu kuhusu matumizi sahihi ya zana za kilimo, usimamizi bora wa ardhi na mbinu zinazoweza kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.
Aidha, amesema NAESA itaimarisha elimu kwa wakulima kuhusu mahitaji ya masoko na mbinu za kuongeza thamani ya mazao, ili waweze kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya walaji na kupata manufaa zaidi ya kiuchumi.
Dkt. Mafuru amesema wakala huo pia unaratibu ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika utoaji wa huduma za ugani, ili kuhakikisha wadau wote wanashirikiana katika kuwafikia wakulima na kuboresha huduma zinazotolewa.
Amesema kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), taarifa za huduma zinazotolewa na maafisa ugani zitaweza kufikishwa kwa wasimamizi, zikionesha afisa aliyetoa huduma, mkulima aliyepatiwa huduma, eneo na muda wa huduma hiyo.
Ameeleza kuwa mfumo huo utasaidia kufuatilia utendaji wa maafisa ugani na kutathmini kama huduma wanazotoa zinachangia kuleta matokeo yaliyokusudiwa katika kuongeza tija na uzalishaji wa wakulima.
Dkt. Mafuru amesema Serikali inaendelea kuwezesha maafisa ugani kwa kuwapatia vitendea kazi ikiwemo pikipiki na magari, ili kurahisisha usafiri na kuwafikia wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
Amebainisha kuwa Agosti 8, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikabidhi magari kwa ajili ya kuratibu shughuli za ugani katika ngazi ya wilaya na halmashauri, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma hizo.
Amesema kuimarishwa kwa NAESA kutasaidia kuhakikisha maafisa ugani wanatambulika, wanawezeshwa na kuwajibika kwa wakulima, huku huduma bora za ugani zikichangia usalama wa chakula, ustahimilivu wa mifumo ya chakula na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Kwa upande wake Mkulima mkongwe kutoka Kijiji cha King’ori, Wilaya ya Meru mkoani Arusha, Mzee Ndetaiywa Nnko, amesema matumizi ya mbegu za kampuni ya Bayer pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo yamemsaidia kuongeza uzalishaji wa mahindi na kuboresha maisha ya familia yake, akivuna hadi gunia 150 kwa msimu katika mashamba yake.
Mzee Nnko, ambaye amewahi kutambuliwa kama Mkulima Bora wa Wilaya ya Meru kwa vipindi vitatu tofauti, amesema kupitia kilimo amefanikiwa kusomesha watoto wake wanane, huku baadhi yao wakiendelea na masomo katika vyuo mbalimbali.
" kwa sasa nimewakabidhi vijana wangu mashamba ili waendelee kujitegemea, na mi nimeamua kusimamia ekari mbili ambazo pia nimekuwa nikizitumia kuonesha kwa vitendo manufaa ya mbegu bora kama balozi wa kampuni ya Bayer, " amesema.
Akielezea matokeo ya uzalishaji katika shamba analolisimamia, Mzee Nnko amesema msimu uliopita alivuna gunia 84 za mahindi, huku msimu wa mwaka huu akipata gunia 72 kutokana na changamoto za hali ya hewa.
Ameongeza kuwa katika mashamba yake mengine amekuwa akipata mavuno ya kati ya gunia 128 na 150, akisisitiza kuwa matumizi ya mbegu bora, elimu ya kitaalamu na kufuata kanuni za kilimo ni mambo muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...