Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Atupele F. Mwakibete, ameongoza kikao cha wadau wa zao la chai kujadili mikakati ya kuendeleza mradi huo wilayani humo, kwa kuweka mazingira bora ya ushirikiano kati ya wakulima na mwekezaji, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha wakulima wananufaika na zao hilo kupitia utaratibu wa haki wa ununuzi na uuzaji wa majani ya chai.
Katika kikao hicho kilichowakutanisha mwekezaji kutoka kampuni ya Hong Ding Xin Investment Limited, wawakilishi wa Bodi ya Chai Tanzania, wakulima na viongozi mbalimbali, Mwakibete amesema Serikali itarejesha mashamba ya chai yaliyotolewa kwa watu ambao hawajayaendeleza ili kuyapatia wawekezaji au watu wenye nia na uwezo wa kuyaendeleza kwa tija.
Amesisitiza kuwa ni muhimu wakulima na mwekezaji kuheshimu makubaliano na mikataba ya kibiashara itakayowekwa ili kuondoa migogoro na kuhakikisha kila upande unatekeleza wajibu wake.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kimeazimia kuwa bei ya ununuzi wa majani ya chai iwe Shilingi 3,000 kwa kilo, huku Bodi ya Chai Tanzania ikitakiwa kuandaa rasimu ya mkataba wa mauziano utakaobainisha bei na masharti ya biashara kati ya wakulima na mwekezaji.
Maazimio mengine ni pamoja na mwekezaji kuwajibika kusafirisha majani ya chai kutoka vituo vya ukusanyaji, Bodi ya Chai kutoa elimu kwa wakulima na wachumaji pamoja na Serikali kushirikiana na wadau kudhibiti changamoto ya moto katika mashamba ya chai.
Aidha, kikao hicho kimependekeza kuwepo kwa mkalimani wa kudumu katika vikao na shughuli zinazomhusu mwekezaji ili kuimarisha mawasiliano na uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa makubaliano.
Akihitimisha kikao hicho, Mwakibete amesisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa ni msingi muhimu wa kuimarisha mradi wa chai Kilolo, kuongeza tija katika uzalishaji na kuhakikisha wakulima wanapata manufaa stahiki kutokana na zao hilo.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...