Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

MKUU wa Wilaya ya Kibaha, Fadhil Emmanuel Nkurlu, amewahakikishia vijana 83 waliohitimu mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba kuwa wilaya itawasiliana na makampuni ya ulinzi na viwanda ili kuwapa kipaumbele katika ajira na kupunguza makali ya ukosefu wa ajira.

Nkurlu ametoa ahadi hiyo wakati akifunga mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba kundi namba 19 mwaka 2026, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Miembesaba, Kibaha mkoani Pwani, Novemba 2, mwaka huu.

Amewataka wahitimu hao kuwa wazalendo, waadilifu na tayari kulitumikia taifa, akisisitiza kuwa mafunzo waliyopata yanapaswa kuwa chachu ya kulinda amani na usalama wa raia pamoja na mali zao, badala ya kutumika kuwatisha wananchi.

"Mafunzo mliyopata yasiwe vitisho mitaani, msiende kutoa mkwala mitaani, nendeni mkawe mabalozi mitaani katika masuala ya amani na usalama kwa raia na mali zao," amesema Nkurlu.

Aidha, amewaasa vijana hao kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vinavyokiuka maadili, huku akiwataka kutumia mafunzo hayo kwa manufaa ya jamii.

Kwa upande wake, Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya , Lt col Katumbi Chinguku amesema mafunzo hayo yalianza Julai mwaka huu, ambapo yalifunguliwa Julai 6 yakiwa na vijana 97.

Chinguku amesema vijana 83 wamehitimu mafunzo hayo, huku 14 wakiacha kutokana na sababu mbalimbali.

Wahitimu hao wameiomba serikali kuwasaidia kupata ajira ili waweze kujikimu kimaisha, wakieleza kuwa kurejea uraiani bila fursa za ajira kutawaacha katika hali ya kuhangaika.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...