BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 2 Novemba, 2026, imefanya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na baadhi ya bandari kavu jijini humo kwa lengo la kujionea miundombinu iliyopo, maendeleo ya uwekezaji na namna inavyosaidia kuongeza ufanisi wa huduma za kibandari.

Ziara hiyo imefanyika katika kipindi ambacho uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam, ukiwemo uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya DP World, umechangia kupunguza msongamano wa mizigo na magari bandarini na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amesema ziara hiyo imewapa Wajumbe wa Bodi fursa ya kujionea miundombinu iliyopo na kuelewa namna inavyosaidia kurahisisha shughuli za kibandari.

Amesema kuwa ufanisi wa bandari unategemea uwepo wa miundombinu bora inayowezesha upokeaji, uhifadhi na uondoshaji wa mizigo kwa wakati, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu na mifumo ya usafirishaji.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya DP World, Bw. Elitunu Mallamia, amesema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za bandari kupitia uwekezaji na maboresho mbalimbali ya miundombinu na mifumo ya uendeshaji.

Naye Mkurugenzi Mkuu na Mmiliki wa Kampuni ya Bravo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, hatua inayochochea ushiriki wa sekta binafsi katika mnyororo mzima wa uwekezaji na utoaji wa huduma za kibandari nchini.

Ziara hiyo imeshirikisha viongozi na watendaji kutoka TASAC, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wadau kutoka Kampuni ya DP World, Kampuni ya TEAGTL, African ICD na Bravo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...