Na. Peter Haule, WF, Dar es Salaam
Finland imeeleza nia ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania kwa kuongeza uwekezaji na shughuli za maendeleo katika sekta za teknolojia ya kidijitali, mawasiliano, misitu na madini.
Hayo yamebainishwa na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Anna Merrifield wakati wa Mkutano na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Merrifield amesema nia ya nchi yake ni kuongeza ushirikiano kutoka katika mfumo wa kawaida wa ushirikiano wa maendeleo na kuelekea katika ushirikiano zaidi unaohusisha pia sekta binafsi, uwekezaji na matumizi ya teknolojia katika kukuza uchumi.
“Finland ina uzoefu mkubwa katika sekta ya teknolojia na ubunifu, hususan katika maeneo ya huduma za kidijitali na mawasiliano, ambayo yanaweza kusaidia Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo”, alisema Mhe. Balozi Merrifield.
Amebainisha kuwa teknolojia ya kidijitali na mawasiliano ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, akisisitiza kuwa maendeleo hayo hayawezi kufikiwa bila matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za uchumi.
Kuhusu ushirikiano na sekta binafsi, amesema Finland inataka kuimarisha uhusiano kati ya miradi ya maendeleo na uwekezaji wa kampuni binafsi, ili kutumia utaalamu wa kampuni za Finland kutatua changamoto za maendeleo nchini Tanzania.
Amesema mkazo utawekwa katika miradi yenye manufaa ya kijamii na kiuchumi ambayo huenda isiweze kujiendesha kibiashara kwa faida ya moja kwa moja, lakini inaweza kuleta matokeo chanya kwa wananchi na kusaidia maendeleo ya Tanzania.
Ameongeza kuwa miradi hiyo inapaswa kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania, huku ikitumia utaalamu na uwezo wa kampuni za Finland kwa manufaa ya pande zote mbili.
Akizungumza awali Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, amesema anafurahishwa na mfumo mpya wa ushirikiano wa uwekezaji katika sekta ya umma (Public Sector Investment Framework – PIF), unaowezesha Tanzania kupata mikopo yenye masharti nafuu inayofadhiliwa kwa ruzuku na Serikali ya Finland kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyokubaliwa.
Amefafanua kuwa mfumo huo unalenga kusaidia miradi ya umma yenye manufaa makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira, ambayo inaweza kukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha kupitia mifumo ya kawaida ya kibiashara.
Akizungumzia utekelezaji wa mfumo huo, alisema mradi wa awali unaotarajiwa kutekelezwa ni Awamu ya Tano ya upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), utakaotekelezwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kwa kushirikiana na kampuni ya Nokia ya Finland.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kufuatilia kwa karibu maandalizi ya mradi huo ili kuhakikisha hatua zinazohitajika zinakamilishwa kwa wakati, akibainisha kuwa nyaraka za mradi huo zinafanyiwa mapitio na Tume ya Taifa ya Mipango.
Dkt. Mwamba ameipongeza Serikali ya Finland kwa ushirikiano wake na kumshukuru Balozi mstaafu wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting, kwa mchango wake katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo, hususan katika kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati.
Mkutano huo ulihudhuliwa pia na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Fedha na Ushirikiano na Sekta Binafsi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Emmi Oikari, Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Nokia, Bw. Amouneu Lopy na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melckizedeck Mbise.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba akiongoza mkutano kati yake na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Anna Merrifield, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, akiagana na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Anna Merrifield, baada ya Mkutano wao kuhusu ushirikiano wa maendeleo, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, Balozi wa Finland nchini, Mhe. Anna Merrifield (wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Finland, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao, uliofanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...