Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Vijijini

WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa la Mlandizi, wilayani Kibaha Vijijini, mkoani Pwani, lenye thamani ya Sh bilioni 7.7, huku akimuagiza mkandarasi kukamilisha mradi huo ifikapo Desemba mwaka huu.

Aidha, amewahakikishia wakandarasi nchini kuwa kuanzia sasa hakutakuwa na kisingizio cha kuchelewesha miradi kutokana na kutolipwa fedha, akisisitiza Serikali imeweka kipaumbele katika ulipaji wa madeni ya wakandarasi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Akizungumza Novemba 21, 2026, wakati wa ziara ya kikazi wilayani Kibaha Vijijini na mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi, Mwigulu aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha gharama za vizimba katika soko hilo hazipandishwi kupita kiasi ili kuepusha kuwakimbiza wafanyabiashara kwa gharama kubwa za upangishaji.

Akizungumzia changamoto ya kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya Makofia-Mlandizi-Mzenga, Waziri Mkuu aliagiza mkandarasi alipwe fedha zinazostahili ili kuendelea na kazi, akieleza kuwa fedha za miradi ya maendeleo, hususan barabara zinazotekelezwa na TARURA na TANROADS, zimeanza kupewa kipaumbele katika utaratibu wa malipo.

“Kuanzia tulipoanza mwaka wa fedha Julai 2026, fedha za miradi ya maendeleo, hasa ya barabara za TARURA na TANROADS, zinakwenda kwenye mifuko ya barabara, hakutakuwa na kusuasua kwa mradi ulioanza utekelezaji, kipaumbele ni kuanza kulipa wakandarasi waliopo site, walioondoa mitambo na wale wanaostahili malipo ya awali,” alisema.

Kuhusu fidia, Mwigulu alisisitiza umuhimu wa wananchi wanaopisha miradi kulipwa kwa wakati ili kupunguza migogoro inayoweza kukwamisha utekelezaji wa miradi, akifafanua kuwa Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu, ikiwemo barabara, katika maendeleo ya wananchi.

Alieleza kuwa ucheleweshaji wa baadhi ya miradi ya barabara haukutokana na uzembe, bali ulitokana na Serikali kuelekeza nguvu na rasilimali katika kukamilisha mradi mkubwa wa kimkakati wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Rufiji, uliokamilika kwa gharama ya Sh trilioni 6.

Mhandisi wa Mkoa, Charles Kabeho, alisema ujenzi wa soko la Mlandizi umefikia asilimia 93, ukiwa na vizimba 770 na majengo manne, huku mradi huo ukitarajiwa kunufaisha wananchi 800.

Alieleza kuwa hadi sasa Sh bilioni 5.132 zimetolewa kwa mradi huo, ambapo mkandarasi amelipwa Sh bilioni 4.543 na majengo yote yako katika hatua za umaliziaji.

Naibu Waziri wa TAMISEMI (Afya), Jafar Seif, alisema mkandarasi ameongezewa muda wa utekelezaji kulingana na makubaliano, hadi Desemba 25 mwaka huu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema barabara inayounganisha Mlandizi-Makofia hadi Maneromango yenye urefu wa kilomita 100 imegawanywa katika vipande vitatu vya utekelezaji, ambavyo ni Makofia-Mlandizi, Mlandizi-Ruvu na Ruvu-SGR-Maneromango.

Alisema kipande cha Makofia kuunganisha barabara kuu, usanifu umekamilika na hatua ya ulipaji fidia imefikia Sh bilioni 8.959, huku Hazina ikiendelea na maandalizi ya malipo.

Kasekenya alieleza kuwa kipande cha Mlandizi-SGR-Ruvu chenye urefu wa kilomita 23 kinatarajiwa kugharimu Sh bilioni 60.250, ambapo mkandarasi ameanza maandalizi na Serikali inaandaa malipo ya awali, huku kipande cha Ruvu-Maneromango usanifu wake ukiwa umekamilika na wananchi wakidai fidia ya Sh bilioni 13.

Awali, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa, aliishukuru Serikali kwa juhudi za kuinua sekta mbalimbali na kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo jimboni humo, huku akitaja changamoto zinazowakabili wananchi kuwa ni ujenzi wa barabara ya Makofia-Mlandizi-Mzenga kwa kiwango cha lami, ulipaji fidia na mkandarasi kukamilishiwa malipo.

Aliomba Ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia ombi la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kupandishwa hadhi na kuwa Mamlaka ya Mji.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...