Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
ONGEZEKO la magonjwa yasiyoambukiza limeendelea kuhitaji juhudi za pamoja katika kuhamasisha jamii kufanya mazoezi mara kwa mara, kuzingatia lishe bora na kufuatilia hali zao za kiafya ili kujikinga na magonjwa hayo.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimekusanya washiriki zaidi ya 700 katika matembezi na mbio za hisani za msimu wa tano zilizofanyika katika kampasi ya chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Bruno Sunguye, amepongeza uongozi wa MUHAS kwa kuandaa matembezi hayo akisema yamewakutanisha wahitimu wa miaka mbalimbali, wanafunzi, wafanyakazi na wadau wa afya kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Amesema shughuli hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya za kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kuzingatia milo bora na kufahamu hali zao za kiafya ili kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.
“Tunawapa hamasa iwe mfano kwa vyuo vingine kuweza kuwa na matukio kama haya ili kwa pamoja tuweze kutengeneza jamii ambayo inakuwa na afya njema na katika harakati za kupambana na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema chuo hicho kitaendelea kutumia matembezi hayo kuhamasisha jamii kujali afya kwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongezeka.
Amesema mwitikio wa washiriki umeendelea kuimarika, ambapo katika msimu huu wamefikia zaidi ya 700, wakiwemo washiriki kutoka Marekani, Ujerumani na Sweden.
Amesema MUHAS pia inaendelea kuboresha miundombinu ya mazoezi katika kampasi yake ya Muhimbili, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo, ukumbi wa mazoezi (gym) pamoja na vyumba vya kuogea na kubadilishia nguo ili kurahisisha ushiriki wa watu katika mazoezi.
Profesa Kamuhabwa amewahimiza wananchi kutumia huduma za uchunguzi wa afya zinazotolewa na taasisi za afya za chuo hicho ili kufahamu hali zao na kupata huduma wanapobainika kuwa na changamoto za kiafya.
Naye Rais wa Convocation ya MUHAS, Marsha Macatta-Yambi, amesema matembezi hayo yana nafasi ya kuwaunganisha wahitimu, wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho, huku yakiimarisha uhusiano wao na chuo hata baada ya kuhitimu.
Amesema msimu wa tano umeonesha maboresho katika ushiriki na udhamini, huku washiriki wakifikia takribani 700 na vifaa vya ushiriki vikiuzwa vyote.
Ameongeza kuwa mapato yanayopatikana kupitia shughuli hiyo huelekezwa katika kusaidia maendeleo ya chuo, ikiwemo kuimarisha mazingira ya wanafunzi na utekelezaji wa mipango mbalimbali kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Ali Hassan Mwinyi wa MUHAS (Ali Hassan Mwinyi MUHAS Endowment Trust Fund).
Amesema matembezi hayo pia yamekuwa fursa ya wahitimu na wanafunzi kukutana, kukumbushana walikotoka na kuendelea kuchangia maendeleo ya chuo hicho.
MUHAS imekuwa ikiandaa matembezi na mbio hizo za hisani kwa misimu mitano mfululizo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kufanya mazoezi na kujenga utamaduni wa kujali afya.
.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...