.jpeg)

.jpeg)
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka, ameitaka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ubunifu, uadilifu na uwezo wa kutatua changamoto zinazolikabili Taifa kupitia teknolojia na mifumo mbalimbali.
Dkt. Isaka amesema wataalamu wanaozalishwa na vyuo wanapaswa kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho la changamoto za jamii kwa kutumia maarifa waliyonayo, ikiwemo kubuni mifumo inayorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema hayo wakati wa Kongamano la Kitaaluma la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa wataalamu kuzingatia uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema pamoja na kuwa na ufaulu mzuri kitaaluma, mtaalamu anapaswa kuwa na maadili na kujitambua ili aweze kutumia ujuzi wake katika kutatua changamoto za wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
“Jamii ina changamoto nyingi ambazo wataalamu wetu wanapaswa kuzitumia kama fursa za kuzitatua kwa kubuni teknolojia na mifumo mbalimbali itakayorahisisha maisha ya watu,” amesema.
Aidha, amesema mabadiliko ya teknolojia na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 yanatoa fursa kwa IFM kuboresha mitaala yake ili kuzalisha vijana wenye uwezo wa ubunifu, uzalishaji na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema NHIF itatoa fursa kwa wanafunzi 10 bora wa mwaka wa tatu wa IFM kufanya mafunzo ya vitendo katika taasisi hiyo ili kuwajengea uzoefu wa kazi na kuwaandaa kwa fursa za ajira na kujiajiri.
Kwa upande wake, Mkuu wa IFM, Profesa Henry Chalu, amesema chuo hicho kitaendelea kuimarisha mifumo ya elimu inayozalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya nchi.
Amesema kongamano hilo ni sehemu ya mkakati wa chuo kuhamasisha tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto katika sekta mbalimbali, huku wanafunzi wakipata fursa ya kuwasilisha mawazo na mifumo waliyoibuni.
Profesa Chalu amesema chuo kinaendelea kusimamia misingi ya elimu inayowawezesha wanafunzi kutumia maarifa yao katika mazingira halisi ya kazi na kujibu mahitaji ya jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Dkt. Shaban Ngole, amesema kongamano hilo limekuwa na mawasilisho mbalimbali yanayolenga kuonesha ubunifu wa wanafunzi na fursa zinazoweza kuwasaidia katika maisha yao ya kitaaluma na kiuchumi.
Amesema wanafunzi 10 wamepata nafasi ya kufanya mafunzo ya vitendo NHIF, hatua itakayowasaidia kuongeza ujuzi na uzoefu katika mazingira ya kazi.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa IFM, Adrian Kachocho, amesema amebuni mfumo unaowasaidia wafanyabiashara kufuatilia mapato na matumizi ya biashara zao, hatua inayoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuboresha usimamizi wa biashara.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...