Shirika la Posta Tanzania limeweka msisitizo mpya katika uwajibikaji kwa kutangaza kuwa utendaji wa mameneja wa mikoa na viongozi wengine utapimwa kwa kuzingatia matokeo ya biashara, ubora wa huduma na uwezo wa kutumia fursa zilizopo kukuza shirika hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Novemba 12, 2026, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa mameneja wa mikoa, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema viongozi watakaoshindwa kutimiza majukumu yao watawajibishwa baada ya tathmini ya utendaji, akisisitiza kuwa hakuna kiongozi atakayebaki nje ya mchakato huo, wakiwemo wa makao makuu.

Mbodo amesema tathmini hizo zitazingatia matokeo ya kila eneo kwa haki, huku watendaji wanaofanya vizuri wakitambuliwa na maeneo yenye changamoto yakifanyiwa uchambuzi kwa lengo la kuboresha utendaji.

Akitolea mfano wa mafanikio, ametaja Mkoa wa Morogoro ambao umepata fursa kubwa ya biashara ya usafirishaji wa vifurushi, kiasi cha kukabiliwa na upungufu wa magari kutokana na ongezeko la mahitaji. Amesema meneja wa mkoa huo ameweka lengo la kusafirisha vifurushi 5,000, hivyo kuitaka menejimenti kutoa rasilimali zinazohitajika.

Katika hatua nyingine, Mbodo amesema Tanzania imepiga hatua katika ushindani wa kimataifa kwa kushika nafasi ya 66 duniani na ya nne barani Afrika katika tathmini ya Umoja wa Posta Duniani (UPU), huku akieleza kuwa shirika hilo linaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha nafasi yake na kuwa kinara wa huduma za posta barani Afrika.

Amewataka mameneja kutumia mafunzo hayo kuboresha usimamizi wa biashara, matumizi ya rasilimali, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wateja, akisisitiza kuwa ukuaji wa Shirika la Posta Tanzania ni jukumu la kila mtumishi.







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...