Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ametoa maelekezo kwa Bodi mpya ya Magavana ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), yakilenga kuimarisha ubora wa elimu na mafunzo, kuongeza ajira kwa mabaharia wa Tanzania na kukifanya chuo kitambulike kimataifa.

Akizungumza katika uzinduzi wa Bodi hiyo, alisema ni mwanzo wa ukurasa mpya wa uwajibikaji, ufanisi na matokeo. Alitaka bodi isimamie uboreshaji wa mitaala, mafunzo kwa wakufunzi na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

Aliitaka bodi, kwa kushirikiana na menejimenti, kuweka mikakati ya kuongeza ajira kwa mabaharia kupitia ushirikiano na kampuni za meli, waendeshaji wa bandari na taasisi za kimataifa, pamoja na mfumo wa kufuatilia maendeleo ya wahitimu.

Pia alisisitiza utawala bora, uwajibikaji na uadilifu, na tafiti na ubunifu vielekezwe katika kutatua changamoto za bandari, usafiri wa majini, usalama baharini na uchumi wa buluu. Aliielekeza DMI kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuandaa kanzidata ya wataalamu wa Kitanzania wa sekta ya bahari waliopo nchini na nje ya nchi.

Aidha, alitaka fedha za Serikali zitumike kwa ufanisi, akionya dhidi ya ucheleweshaji, ongezeko la gharama lisiloelezeka na ununuzi wa vifaa visivyokidhi viwango, na akahimiza chuo kuongeza mapato kupitia mafunzo, tafiti na huduma za ushauri, kwa kuzingatia malengo yanayopimika na muda maalumu wa utekelezaji.

Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Mkuu Paul Olekashe, alitaja changamoto kuwa ni upatikanaji wa meli ya mafunzo, vifaa vya kisasa na utambuzi wa vyeti vya mabaharia kimataifa. Alisema chuo kinaandaa mradi wa meli ya mafunzo, na akaiomba Wizara kuharakisha utekelezaji wake na kusaidia vyeti vitambuliwe kimataifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo, Profesa Tumaini Gurumo, alisema wanafunzi wa mafunzo ya bahari wameongezeka kutoka 1,500 hadi 7,000 kwa mwaka, huku idadi ya walimu ikiongezeka kutoka chini ya 100 miaka mitano iliyopita hadi takribani 220 sasa, aliongeza kuwa Serikali inaendelea kukiimarisha chuo kwa kukipatia vifaa vya kisasa vya kufundishia ili kuboresha ubora wa mafunzo.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...