Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema imejipanga kuyawezesha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ya ndani kupata vyanzo vya fedha nchini ili kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje na kuhakikisha yanaendelea kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya wananchi.

Hatua hiyo inafuatia uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund - NBF), unaolenga kuimarisha uendelevu wa sekta hiyo kupitia rasilimali za ndani ya nchi.

Hayo yameelezwa katika kikao cha pili cha Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Uanzishwaji wa Mfuko huo, kilichofunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, ambapo wajumbe walijadili hatua zilizofikiwa na mikakati ya kuhakikisha mfuko huo unakamilika kwa wakati.

Akizungumza katika kikao hicho, Maswi amesema nchini kuna zaidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali 8,000, lakini mengi yanategemea misaada kutoka nje ya nchi, hivyo Serikali ina wajibu wa kuangalia namna ya kuyawezesha mashirika ya kitaifa kupata rasilimali za ndani ili yaweze kutekeleza shughuli zake nchini.

"Serikali inayachukulia mashirika haya kama washirika muhimu katika shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mpango wa pamoja utakaowezesha upatikanaji wa fedha za kusaidia utekelezaji wa majukumu yao"
Kwa upande wake, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vickness Mayao, amesema maagizo ya kuanzisha mfuko huo yalilenga kuwakutanisha wadau ili kuandaa utaratibu maalumu wa kusaidia mashirika ya ndani, hatua iliyosababisha kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Uanzishwaji wake.

Mayao amesema kamati hiyo inaongozwa na Dkt. Majid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, na tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha mfuko huo unaanza kufanya kazi mapema ili mashirika ya ndani yanufaike na rasilimali zilizopo nchini.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania, Jasper Makala, amesema mfuko huo unatarajiwa kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya nchi, ambao umekuwa ukipungua kadri siku zinavyokwenda.

Amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yana mchango mkubwa katika maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii katika sekta mbalimbali, hivyo upatikanaji wa mfuko wa ndani utayasaidia kujiendesha kwa uendelevu na kuendelea kuwahudumia wananchi.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...