Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amekabidhi rasmi Cheti cha Usajili kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (TACOEJ), huku akiahidi kushirikiana na chama hicho kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa pamba.
Mtanda amekabidhi cheti hicho leo Novemba 3, 2026 ofisini kwake, mara baada ya kutembelewa na viongozi wa chama hicho.
Akizungumza baada ya kukabidhi cheti hicho, Mtanda amesema pamba ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Simiyu, na kwamba kama Mkuu wa Mkoa anapaswa kujifunza kwa haraka changamoto zinazolikabili zao hilo.
"Pamba ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Simiyu. Zao hili lina changamoto nyingi sana na mimi kama Mkuu wa Mkoa ninatakiwa kujifunza haraka ili nijue changamoto za zao la pamba," amesema Mtanda.
Ameongeza kuwa Serikali imeagiza kufanyika kwa vikao vya wadau kabla ya msimu, na kwamba badala ya kongamano peke yake, ni vyema wadau wakashirikiana kuandaa kikao cha wadau wa pamba ili waandishi wawe sehemu ya wadau na kutumia kalamu zao kufikisha elimu kwa umma kuhusu maazimio yatakayofikiwa.
Amesema lengo ni kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji kutoka tani 133,000 hadi kufikia tani 200,000, kwa kushirikiana na waandishi wa habari za pamba na mazingira ili jamii ifahamu umuhimu wa pamba katika uchumi wa Simiyu.
Pia amesema atahakikisha wanakutana mara kwa mara na wadau wengine wa sekta ndogo ya pamba na mazingira ili changamoto za zao hilo zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Awali, Katibu wa TACOEJ, Sitta Tumma, amesema chama hicho kitatumia taaluma yake ya uandishi wa habari kuhakikisha elimu sahihi ya kilimo cha pamba inawafikia wakulima ili waongeze tija katika uzalishaji.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...