Na Khadija Kalili, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, kuhakikisha zinaundwa kamati za usuluhishi na utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji ili kuimarisha mahusiano na kudumisha amani katika maeneo yenye changamoto hizo.
Amesema kamati hizo zitakuwa na jukumu la kusikiliza pande zinazohusika, kusuluhisha migogoro na kutafuta ufumbuzi wa kudumu, sambamba na kuweka utaratibu wa kuchukua hatua stahiki dhidi ya wanaokiuka makubaliano na taratibu zilizowekwa, kwa lengo la kuhakikisha makundi hayo yanaishi kwa maelewano na kuheshimiana.
Mhe. Nyongo ametoa agizo hilo Novemba 2, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Fukayosi, Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, ulioitishwa kufuatia mgogoro baina ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamang’ati katika eneo hilo.
Katika mkutano huo, amewataka wafugaji kuacha mara moja tabia ya kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji, ili kila kundi liweze kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Aidha, amewataka wakulima kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kuwadhuru wafugaji au mifugo yao, akisisitiza kuwa migogoro inapaswa kutatuliwa kupitia vyombo na mifumo halali badala ya kutumia nguvu.
Akizungumzia madai ya baadhi ya wafugaji kuwa wameinunua Serikali, Mhe. Nyongo amekemea vikali kauli hizo na kusisitiza kuwa Serikali haiko chini ya mtu au kundi lolote, hivyo haitasita kuwachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kusababisha vurugu.
“Naomba niwashukuru kwa taarifa mlizonipatia. Nitazifuatilia moja baada ya nyingine, na nikibaini kuna kiongozi yeyote anayehusika na vitendo hivyo, nitamshughulikia ipasavyo. Ninachotaka ni wananchi waishi kwa amani,” amesema RC Nyongo.
Akizungumzia suala la ulinzi na usalama, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, hususan wanapohitajika kutoa ushahidi mahakamani, ili kuhakikisha kesi zinazohusu migogoro hiyo zinafuatiliwa hadi zinapotolewa maamuzi kwa mujibu wa sheria.
“Ikipelekwa kesi mahakamani, hakikisheni mnaifuatilia kwa kutoa ushirikiano unaostahili hadi pale kesi itakapomalizika. Hatuwezi kujenga amani kama wananchi wenyewe hatutakuwa tayari kushiriki katika kuhakikisha haki inatendeka,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Mhe. Nyongo amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani kuhakikisha askari wanaokiuka maadili na wajibu wao wanachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za Jeshi hilo.
Pia, amemtaka kuimarisha Kituo cha Polisi Kiwanga kwa kuongeza idadi ya askari wa doria ili kuimarisha ulinzi na usalama na kudhibiti vitendo vinavyoweza kuvuruga amani katika maeneo hayo.
Vilevile, amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kutekeleza wajibu wao kwa kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi badala ya kuwa chanzo cha migogoro na mifarakano katika jamii.
“Sitavumilia kiongozi au mtu yeyote anayehatarisha usalama wa wananchi. Sitaki kuona wananchi wanakosa amani,” amesisitiza Mhe. Nyongo.
Ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatambua amani kuwa msingi muhimu wa maendeleo, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kulinda utulivu, kuheshimu sheria na kushiriki katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, hususani katika hatua za uchunguzi na uendeshaji wa kesi Mahakamani, akieleza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakisita kutoa ushahidi wanapohitajika.
Amesema ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha wanaohusika na vitendo vya uvunjifu wa sheria wanachukuliwa hatua stahiki, hatua itakayosaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika jamii.


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...