Serikali imelielekeza Shirika la Posta Tanzania kuhakikisha vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vilivyokabidhiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) vinatumika ipasavyo katika kuboresha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza ufanisi na kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia yanayoendana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Switbert Mkama, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa Shirika la Posta Tanzania kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu ya kubadilisha na kuboresha huduma zake.

Dk. Mkama amesema mashirika ya posta duniani yanapitia mabadiliko makubwa ya kiutendaji, yakitoka katika mfumo wa kutoa huduma za usafirishaji wa barua pekee na kuelekea kuwa vituo vya kisasa vinavyotoa huduma mbalimbali za kidijitali.

Amesema kwa sasa mashirika hayo yanapanua wigo wa shughuli zake kwa kujumuisha biashara mtandao, huduma za kifedha na ujumuishaji wa wananchi katika mifumo ya kifedha, pamoja na huduma za Serikali mtandao.

Ameeleza kuwa mabadiliko hayo yanaonesha umuhimu wa Shirika la Posta Tanzania kuimarisha matumizi ya teknolojia katika shughuli zake ili kuendana na mahitaji ya sasa ya wananchi, kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha nafasi yake katika uchumi wa kidijitali.

Aidha, amesema uwekezaji katika vifaa vya TEHAMA ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kisasa na shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha uchumi wa kidijitali kwa kuhakikisha teknolojia inatumika kuboresha utendaji wa taasisi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Mlembwa Mnakua, amesema mfuko huo umeendelea kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania katika kuimarisha uwezo wake wa kiteknolojia, ambapo katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka wa fedha uliopita, umewezesha ununuzi wa vifaa kwa ajili ya shirika hilo vyenye thamani ya Sh bilioni 2.5.

Mnakua amesema uwekezaji huo unalenga kuongeza uwezo wa shirika kutumia mifumo ya kisasa katika shughuli zake na kuboresha upatikanaji wa huduma za posta kwa wananchi.

Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, UCSAF imetenga Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa zaidi vya TEHAMA pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kutolea huduma za posta.

Amesema mpango huo unalenga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma hizo na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini, ili nao wanufaike na maendeleo ya teknolojia na huduma zinazotolewa na Shirika la Posta.

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema shirika hilo limejipanga kuhakikisha vifaa vilivyokabidhiwa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Mbodo amesema shirika litatumia vifaa hivyo kuimarisha mifumo yake ya utoaji huduma, huku likihakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yanayotarajiwa na kuchangia kuboresha huduma kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesisitiza kuwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini, wanatarajiwa kunufaika na juhudi hizo kupitia kuimarishwa na kusogezwa karibu kwa huduma za posta.

Hatua hiyo inaonesha mwendelezo wa juhudi za Serikali na UCSAF katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA na kuongeza matumizi ya teknolojia katika taasisi za umma, ili Shirika la Posta Tanzania liweze kupanua huduma zake na kuendana na mabadiliko ya uchumi wa kidijitali.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...