
Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha uhifadhi, kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi na kupanua mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa, huku likilenga kuhakikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wananufaika na rasilimali zilizopo.
Mikakati hiyo inajumuisha kuboresha miundombinu ya usafiri, matumizi ya teknolojia za kisasa katika ulinzi wa wanyamapori, kuimarisha huduma za utalii na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii zinazozunguka hifadhi.
Akizungumza katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 10, 2026, Kamishna wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa, alisema ujenzi wa viwanja vinne vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi na Ruaha, ambako viwili vinajengwa, pamoja na uwekezaji wa Serikali katika reli ya kisasa ya SGR na kuboresha barabara, umeongeza urahisi wa kufikika kwa hifadhi hizo.
Alisema maboresho hayo yanaongeza mvuto wa hifadhi za taifa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi, kutokana na kurahisisha safari na kupunguza changamoto za usafiri.
Katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali za taifa, Mwishawa alisema TANAPA imeongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika doria, ufuatiliaji wa wanyamapori na kudhibiti vitendo vya ujangili.
Aliongeza kuwa wananchi wamewezeshwa kutoa taarifa za matukio yanayohusisha wanyamapori wakali na waharibifu kupitia namba maalumu za mawasiliano zilizowekwa katika kanda mbalimbali za Shirika.
Akizungumzia manufaa ya uhifadhi kwa jamii, alisema TANAPA inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wanaozunguka hifadhi, ikiwemo ujenzi wa shule, mabweni, zahanati na vituo vya polisi, uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa ya maji.
Alisema pia Shirika limewezesha uanzishwaji wa viwanda vidogo vya kukamua mafuta ya alizeti na kusindika asali ili kuongeza thamani ya mazao na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, alisema TANAPA inaendelea kuwawezesha wananchi kupitia vyama vya kuweka na kukopa vya kijamii (COCOBA), vinavyowapatia mikopo ya fedha na mitaji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Alisema mpango huo umesaidia wananchi kujiajiri, kuanzisha biashara na kuongeza kipato, akisisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni msingi muhimu wa mafanikio ya uhifadhi endelevu.
Katika kupanua wigo wa utalii, Mwishawa alisema TANAPA imewekeza pia katika uwanja wa gofu uliopo Fort Ikoma, pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa lengo la kuunganisha utalii wa wanyamapori na michezo.
Alisema uwanja huo unatarajiwa kuvutia wapenzi wa mchezo wa gofu na watalii wa hadhi ya juu kutoka masoko ya kimataifa, sambamba na kuongeza fursa za uwekezaji na kuitangaza Tanzania katika utalii wa gofu duniani.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka mkazo katika kukuza utalii Kusini na Magharibi mwa nchi kwa kuvutia uwekezaji katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Ruaha, Kitulo, Katavi, Gombe, Milima ya Mahale, Milima ya Udzungwa na Rubondo.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, inayolenga kutumia rasilimali zilizopo kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira.
Katika kutumia fursa za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Mwishawa alisema TANAPA kwa kushirikiana na wadau wa utalii imepanga kuandaa vifurushi maalumu vya utalii vitakavyowawezesha mashabiki wa soka wanaotembelea Tanzania kutembelea hifadhi mbalimbali.
Alizitaja hifadhi hizo kuwa ni Serengeti, Nyerere, Saadani, Mikumi, Tarangire, Arusha na Manyara.
Alisema mpango huo utawapa mashabiki wa soka fursa ya kujionea vivutio vya utalii katika siku ambazo hawatakuwa viwanjani kushuhudia mechi, huku ukilenga kuongeza idadi ya watalii na mapato ya Taifa.
Mikakati mingine iliyotajwa ni ujenzi wa barabara ya kilomita 6.69 kwa kiwango cha lami kutoka lango kuu la Hifadhi ya Taifa ya Manyara hadi Minjingu, pamoja na kuanzisha utalii wa majini katika Ziwa Victoria.
Alisema utalii huo wa majini utaunganisha Hifadhi ya Serengeti kupitia Ghuba ya Speke, Kisiwa cha Saanane, Kisiwa cha Rubondo na Hifadhi ya Burigi-Chato.
Akizungumzia mwenendo wa utalii katika mwaka wa fedha 2025/2026, Mwishawa alisema TANAPA imeendelea kuimarisha ushindani wa hifadhi za taifa katika soko la kimataifa, kukuza utalii wa ndani, kuboresha huduma na kupanua wigo wa uwekezaji.
Alisema hatua hizo zinalenga kuongeza mapato ya Serikali na mchango wa sekta ya utalii katika upatikanaji wa fedha za kigeni.
Katika hatua nyingine, aliwataka wahariri na waandishi wa habari kuwa washirika muhimu wa TANAPA katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Pia aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za hifadhi, kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohatarisha maliasili na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na shughuli za utalii ili kujiongezea kipato.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...