
NA MWANDISHI WETU - ARUSHA
Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha usalama wa mionzi kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu (IAEA) na Umoja wa Ulaya (EU), kupitia mafunzo ya kikanda yanayolenga kuwajengea uwezo wataalamu katika uandaaji wa viwango maalum vya usalama wa mionzi kwa vifaa vinavyokusudiwa kutumika tena, kuchakatwa au kutupwa.
Mafunzo hayo ya siku tano, yanayofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 16 hadi 20 Novemba 2026, yanalenga kuimarisha uwezo wa nchi katika kufanya tathmini ya viwango vya mionzi kwenye vifaa mbalimbali ili kuhakikisha kuwa matumizi yake hayaleti madhara kwa afya za binadamu na mazingira.
Akifungua mafunzo hayo leo, Novemba 16, 2026, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia, Dkt. Harun Makandi, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu na mifumo ya udhibiti wa usalama wa mionzi, hususan katika kipindi ambacho matumizi ya teknolojia ya nyuklia na vyanzo vya mionzi yanaendelea kuongezeka katika sekta mbalimbali.
Dkt. Makandi ameeleza kuwa uandaaji wa viwango maalum vya kuondoa vifaa kwenye udhibiti wa mionzi (Specific Clearance Levels) ni hatua muhimu inayowezesha kufanya maamuzi ya kitaalamu kuhusu vifaa vinavyoweza kutumika tena, kuchakatwa au kutupwa bila kuhatarisha usalama wa wananchi, wafanyakazi na mazingira.
Katika mafunzo hayo, washiriki watajifunza masuala mbalimbali yakiwemo misingi ya ulinzi dhidi ya mionzi, taratibu za kuandaa viwango maalum vya usalama, tathmini ya athari zinazoweza kutokana na mionzi pamoja na matumizi ya mbinu za kitaalamu katika kufanya maamuzi kuhusu usimamizi wa vifaa vyenye mionzi.
Aidha, mafunzo hayo yanatoa fursa kwa wataalamu kutoka nchi mbalimbali kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kuhakikisha kuwa viwango vya usalama wa mionzi vinazingatiwa kwa mujibu wa miongozo na viwango vya kimataifa.
Mafunzo hayo yanahusisha wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu (IAEA), Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Nishati ya Nyuklia la Afrika Kusini (NECSA) pamoja na washiriki kutoka nchi mbalimbali, huku Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ikiwa mwenyeji wa mafunzo hayo.
Kupitia mafunzo hayo, Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake katika usimamizi wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na mionzi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na kulinda mazingira, wafanyakazi, wagonjwa na wananchi dhidi ya madhara ya mionzi.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...