Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa Kitambulisho cha Taifa Kilichoboreshwa, toleo la mwaka 2026, utakaofanyika Novemba 18, katika Viwanja vya Stendi ya zamani ya Maili Moja, Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, alisema Waziri Mkuu atakuwa mkoani humo Novemba 18 na 21 mwaka huu ambapo baada ya uzinduzi huo atafanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Manispaa ya Kibaha.
Nyongo amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa utambulisho wa Taifa, kuongeza ufanisi wa utambuzi wa watu, kuimarisha usalama wa taarifa za wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma zinazohitaji utambulisho rasmi.
Ameeleza sambamba na uzinduzi huo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) itazindua huduma mpya ya Huduma Bila Foleni, inayolenga kupunguza muda wa wananchi kusubiri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Amefafanua kuwa wananchi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Pwani watapata huduma mbalimbali katika eneo la uzinduzi, zikiwemo usajili wa ambao hawajajisajili, uhakiki na marekebisho ya taarifa, ufuatiliaji wa maombi pamoja na utoaji wa vitambulisho vilivyokamilika kwa wenye namba za utambulisho wa Taifa ambao hawajavichukua.
Vilevile, wananchi watapata elimu na ushauri kuhusu taratibu na huduma zinazotolewa na NIDA, huku akiwahimiza kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo na kushiriki mkutano wa hadhara utakaofanyika baada ya uzinduzi.
Katika hatua nyingine, Nyongo amesema Novemba 21 mwaka huu, Waziri Mkuu atafanya ziara katika Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo, ambako atafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Polisi Chalinze.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...