Na Mwandishi Wetu, WMTH – Singapore.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ametoa wito wa kuimarisha uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali barani Afrika kupitia ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Asia ili kuharakisha ukuaji wa uchumi.
Wito huo umetolewa katika Mazungumzo ya Uwekezaji wa Miundombinu kati ya Afrika na Singapore (Africa-Singapore Infrastructure Investment Dialogue), yaliyofanyika Singapore na kuwakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji na taasisi za fedha kujadili fursa za uwekezaji katika miundombinu.
Waziri Kairuki amesema teknolojia na mawasiliano ni sehemu muhimu ya miundombinu ya sekta mbalimbali, ikiwemo nishati, bandari na usafirishaji, hivyo zinapaswa kupewa kipaumbele sawa na miundombinu mingine ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa kuimarisha ubia kati ya serikali na sekta binafsi za Afrika na Asia kutasaidia kuvutia mitaji, teknolojia na utaalamu, kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Taifa wa Singapore, Bw. Alvin Tan, amesema nchi hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano na Afrika katika miundombinu, nishati, usafirishaji, uchumi wa kidijitali na teknolojia za fedha. Pia, ametaja majadiliano kuhusu Mkataba wa Biashara Huria kati ya Singapore na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mazungumzo hayo pia yalijadili njia bunifu za ufadhili wa miradi na kuimarisha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), huku Jukwaa la Biashara kati ya Afrika na Singapore likitarajiwa kufanyika Julai 2027, likitoa fursa zaidi za kukuza uwekezaji na biashara baina ya kanda hizo.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...