Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limeiomba Serikali kuimarisha mfumo wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala nchini kwa kuwekeza katika elimu, tafiti za kisayansi, udhibiti wa ubora wa dawa, uhifadhi wa mimea tiba na uwekezaji katika sekta hiyo.

Katika waraka wa mapendekezo ya kimkakati uliotolewa Novemba 2026, TRAMEPRO imependekeza Tanzania kujifunza kutoka Jamhuri ya India, ambayo imepiga hatua katika kurasimisha na kuendeleza mifumo ya tiba za jadi kupitia Wizara maalumu ya AYUSH.

Shirika hilo limeeleza kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa mimea tiba na maarifa ya jadi yaliyorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, lakini bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili sekta hiyo iweze kuchangia kikamilifu katika afya ya jamii na uchumi wa taifa.

Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa ni upungufu wa tafiti za kisayansi, mifumo ya mafunzo na viwango vya kitaaluma, vifaa vya kupima ubora wa bidhaa, pamoja na uharibifu wa mazingira unaosababisha kupungua kwa baadhi ya mimea tiba.

TRAMEPRO imependekeza pia kuimarishwa kwa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa kuongeza rasilimali watu, fedha, vifaa na mifumo ya kidijitali ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Aidha, shirika hilo limetaka kuanzishwa kwa mfumo wa mafunzo ya kitaaluma utakaowawezesha wataalamu wa tiba asili kupata elimu ya kisasa kuhusu usalama wa wagonjwa, matumizi sahihi ya dawa, maadili ya taaluma na umuhimu wa kuwapeleka wagonjwa kwenye huduma za kisasa pale inapohitajika.

Katika eneo la utafiti, TRAMEPRO imependekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), vyuo vikuu, taasisi za afya na wataalamu wa tiba asili ili kuchunguza kisayansi mimea tiba, viambato vyake, usalama na ufanisi wake.

Kwa upande wa uchumi, shirika hilo limehimiza Serikali kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mimea tiba, maabara za kupima ubora, uzalishaji wa bidhaa zenye viwango na upanuzi wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, TRAMEPRO imependekeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kuanzisha mazungumzo rasmi na Wizara ya AYUSH ya India ili kuwezesha kubadilishana uzoefu, mafunzo, teknolojia, tafiti za pamoja na fursa za uwekezaji.

Waraka huo pia unapendekeza utekelezaji wa mpango wa miaka mitano kuanzia 2027 hadi 2031, utakaoanza na tathmini ya mfumo uliopo, kuimarisha taasisi na mifumo ya udhibiti, kuendeleza tafiti na uzalishaji, kukuza uwekezaji na hatimaye kufanya tathmini ya matokeo.

TRAMEPRO imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kupokea na kutathmini mapendekezo hayo, kuitisha mkutano wa kitaifa wa wadau wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Sura ya 244.

Akieleza msimamo wa shirika hilo, Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura F. Mwalongo, amesema maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kujengwa kwa ushirikiano wa Serikali, wataalamu, taasisi za utafiti, vyuo vikuu na sekta binafsi.

Amesisitiza kuwa lengo la mapendekezo hayo si kuiga mfumo wa India, bali kujifunza kutokana na uzoefu wake na kujenga mfumo wa Tanzania unaozingatia mazingira, rasilimali na mahitaji ya nchi.

Kauli mbiu ya waraka huo ni: “Tuisimamie Tiba Asili kwa Maarifa, Tuiendeleze kwa Sayansi, Tuilinde kwa Sheria na Tuikuze kwa Uchumi.”

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...