Meneja wa Masuala ya Uendelevu wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita ( GGML) Bw. Gilbert Mworia akizungumza wakati wa mkutano wa kufanya tathmini ya fedha za GGM Kili Challenge against HIV & AIDS uliojumuisha taasisi zilizopata fedha hizo kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Bi Neema Julius kutoka Taasisi ya Konga la Waviu Arusha akiwasilisha namna taasisi hiyo ilivyonufaika na mgao wa fedha zilizotolewa na kampeni ya GGM Kili Challenge Against HIV & AIDS wakati wa tathmini ya kikao kinachoendelea Moshi, mkoani Kilimanjaro
Bi Neema Julius kutoka Taasisi ya Konga la Waviu Arusha akiwasilisha namna taasisi hiyo ilivyonufaika na mgao wa fedha zilizotolewa na kampeni ya GGM Kili Challenge Against HIV & AIDS wakati wa tathmini ya kikao kinachoendelea Moshi, mkoani Kilimanjaro
Wadau wakifatilia mada
Na Mwandishi Wetu
MOSHI, KILIMANJARO – GGM Kilimanjaro Challenge Against HIV & AIDS Trust kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeanza kufuatilia utekelezaji wa miradi ya taasisi/mashirika zilizopokea fedha kupitia kampeni hiyo kwa msimu wa mwaka 2025/26 ili kutathmini mafanikio, changamoto na matokeo ya uwekezaji huo katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.
Ufuatiliaji huo unafanyika kupitia semina ya siku mbili katika Hoteli ya Weruweru, jijini Moshi, mkoani Kilimanjaro, itakayofuatiwa na ziara ya siku tatu katika maeneo mbalimbali yanakotekelezwa miradi ya taasisi/mashirika hayo.
Akizungumza katika semina hiyo, Mwenyekiti wa Timu ya Ufundi, ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa TACAIDS, Bw. Nyangusi Laiser, alisema rasilimali zinazopatikana kupitia kampeni hiyo ni muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.
Alisema licha ya hatua zilizopigwa katika kupunguza maambukizi, ugonjwa huo bado ni changamoto, huku vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wakiwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi.
Aliongeza kuwa wanawake ndio kundi lilioathiriwa zaidi, likiwakilisha asilimia 80 ya maambukizi yote nchini, yanayohusisha watu 1,548,000, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023.
“Wote tunafahamu kuwa rasilimali fedha kutoka kwa mashirika ya kimataifa zilizokuwa zikitumika kusaidia mapambano dhidi ya UKIMWI barani Afrika zimepungua.
Hivyo, kampeni hii inayosimamiwa na GGML kwa zaidi ya miaka 24 ni muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kutokomeza ugonjwa huu nchini,” alisema Bw. Laiser.
Katika uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji, taasisi zilizopokea fedha kupitia kampeni hiyo zilieleza kuwa ufadhili huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya watu wanaoishi na VVU na UKIMWI.
Aliisema fedha hizo zimewezesha kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya kuongeza kipato, kutoa elimu kuhusu kujikinga na maambukizi mapya, kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV) na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC).
Akielezea mafanikio ya mradi wao, Afisa wa Kikundi cha Jali Afya Yako, Epuka Maambukizi Mapya, Fuata Ushauri na Nasaha (KIJAEFA), Bw. Roymen Siria, alisema taasisi hiyo kupitia kampeni hiyo ya mwaka 2025/26 ilipokea mgao wa Sh milioni 30 ambazo zimewekezwa katika mradi wa uzalishaji wa unga wa lishe kwa ajili ya kuimarisha afya ya jamii na kuongeza kipato cha wanufaika.
“Tumewekeza katika ununuzi wa vifaa mbalimbali na kuanzisha uzalishaji wa unga wa lishe kama njia ya kujiongezea kipato na wakati huohuo kuchangia kuboresha afya ya jamii,” alisema Bw. Siria.
Alisema kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kusajili bidhaa zao katika taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili ziweze kukidhi vigezo vinavyohitajika na kuingia katika masoko ya kitaifa na kimataifa.
Aliongeza kuwa ukosefu wa kipato ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili watu wanaoishi na VVU, hivyo mradi huo unalenga kuwapatia fursa za kiuchumi zitakazowasaidia kujitegemea na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Bi. Neema Julius kutoka taasisi ya Konga la Waviu Arusha, ambayo pia ni mnufaika wa fedha hizo, alisema taasisi yao imejikita katika kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI, kuhamasisha upimaji wa afya katika kaya na kuwaunganisha watu wanaobainika kuwa na maambukizi na huduma stahiki za matibabu.
“Taasisi yetu inajikita zaidi katika kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI, kufanya upimaji wa afya katika kaya na kutoa rufaa kwa watu wanaobainika kuwa na maambukizi ili waweze kupata huduma sahihi katika vituo vya afya,” alisema Bi. Julius.
Alisema ufadhili huo umeongeza uwezo wa watoa huduma wa taasisi hiyo kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutoa elimu inayolenga kupunguza maambukizi mapya na athari za VVU na UKIMWI katika jamii.
Akizungumzia mchango wa kampeni hiyo, Meneja wa Kili Trust, Bw. Stephen Mhando, alisema fedha zinazotolewa kwa taasisi hizo zinatokana na kampeni ya kuchangisha fedha kupitia kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro inayofanyika kila mwaka kwa njia ya miguu na baiskeli.
Alisema kampeni hiyo inalenga kukusanya rasilimali fedha kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa afua mbalimbali za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali.
“Tumeendesha kampeni hii kwa zaidi ya miaka 24 sasa, huku ushirikiano wetu na TACAIDS ukiwa umeanza mwaka 2014. Lengo letu ni kuhakikisha ndoto ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vinavyotokana na Ukimwi inatimia,” alisema Bw. Mhando.
Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na michango ya taasisi na mashirika mbalimbali, bado kuna haja ya wadau kuendelea kushirikiana kwa kuwa maambukizi ya VVU bado yapo nchini.
“Ni muhimu wadau wote tuendelee kushikana mikono na kuimarisha juhudi hizi ili kuifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya VVU na UKIMWI,” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Uendelevu wa GGML, Bw. Gilbert Mworia, alisema upatikanaji wa rasilimali fedha ni nguzo muhimu katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, akizitaka taasisi, mashirika na vikundi vinavyotekeleza afua mbalimbali kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayoviwezesha kupata fedha dhidi ya mapambano hayo.
Alisema hatua hiyo itasaidia taasisi hizo kuendelea kutoa huduma kwa jamii hata pale ufadhili kutoka nje unapopungua au kukosekana.
“Tunawashauri kutumia fursa ya uwezeshaji unaotokana na kampeni ya GGM Kili Challenge kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowapatia rasilimali fedha, ili muweze kuendelea kuhudumia jamii katika maeneo yenu hata kama ufadhili kutoka nje utapungua au kukatika,” alisema Bw. Mworia.
Akifafanua kuhusu madhumuni ya semina na ziara hiyo, Afisa Utawala wa kampeni ya Kili Challenge, Bi. Njile Mabula, alisema kukutana na taasisi wanazozisaidia pamoja na kutembelea maeneo yao ya utekelezaji ni utaratibu wa kila mwaka unaolenga kutathmini maendeleo ya miradi hiyo.
Alisema ziara hizo pia hutoa fursa ya kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika ipasavyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...