Na George Maziku, Geita

Imeelezwa kuwa kampuni za kigeni za uchimbaji madini ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kiufundi na kifedha wachimbaji wa kitanzania, hivyo wanapaswa kukaribishwa vizuri badala ya kujengewa chuki.

Hayo yameelezwa na mwakilishi wa mkurugenzi wa mgodi wa Peter Kisula Kawe and Partiners, Naomi Mabula alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni.

Mgodi huo uliopo katika kijiji cha Kelezia, kata ya Igulwa, wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, uliingia mkataba wa ubia na kampuni ya Tanzania-Zambia Ding Tai Mining inayomilikiwa na raia wa China.

Mabula alisema kuwa mara baada ya kupewa leseni ya utafiti na uchimbaji madini katika kijiji cha Kelezia, waliamua kutafuta mbia wa kushirikiana nao kwakuwa uwezo wao wa kifedha, kiufundi na kiteknolojia ulikuwa mdogo hivyo wasingezalisha kwa ufanisi.

"Uamuzi wa kutafuta wabia kutoka nje ili kushirikiana katika uchimbaji ulitokana na ukweli kwamba sisi uwezo wetu wa kuchimba ulikuwa mdogo tusingeweza kucbimba kwa ufanisi. Hawa wachina tunaendelea nao vizuri, wanafuata vipengele vyote vya mkataba vinavyowahusu, nasi kwa upande wetu tunatimiza majukumu yetu ya kimkataba, kwa ujumla pande zote za mkataba tunanufaika", alifafanua Mabula.

Aliongeza, "Ushauri wangu kwa wacbimbaji wenzetu waliopewa leseni na serikali ni kwamba wawe makini wanapotafuta wabia wa kushirikiana nao kwa kuajiri wanasheria wazuri ili kulinda kikamilifu maslahi yao", alishauri Mabula.

Akizungumzia kuhusu usalama wa mgodi huo hususani katika kipindi hiki cha mvua, Mhandisi mkuu wa mgodi huo Moses Andrew aliwahakikishia usalama wafanyakazi, wamiliki wa migodi na mitambo ya uchenjuaji waliopo jirani, na jamii nzima inayozunguka mgodi huo.

Mhandisi huyo alisema kuwa mgodi wake umechukua tahadhari zote za kiusalama ikiwemo kuchimba na kuimarisha mitaro mikubwa inayozunguka eneo lote la mgodi, kuimarisha mabwawa wanayotumia kuchenjulia dhahabu, pamoja na kuendelea kutoa mafunzo ya kiusalama kwa wafanyakazi wote wa mgodi wake.

"Hatutegemei kupata ajali ya kiusalama, tumejiandaa vizuri sana na tumechukua hatua zote muhimu za kuhakikisha usalama kwa wafanyakazi wetu wote, majirani zetu wote wanaofanya kazi za madini kama sisi, na jamii yote ya hapa Kelezia. Ninawaambia wasihofu kuhusu usalama wao", alibainisha mhandisi huyo.

Akifafanua zaidi kuhusu usalama wa mgodi wake, mhandisi huyo alisema kuwa pamoja na matumizi ya kemikali kali zinazotumika kurutubisha na kuchenjua dhahabu, lakini hakuna madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali hizo kwani mifumo iliyowekwa hairuhusu maji yenye sumu kutawanyika.

"Hayo maji yenye sumu yamedhibitiwa kikamilifu yasitawanyike kwasbabu yamebeba dhahabu nyingi, kuyaacha yatawanyike kiholela ni hasara kubwa. Isitoshe kiwango cha sumu kinachotumika kimeruhusiwa kisheria, ni cha kiwango cha chini ili kuepuka madhara kama kwa bahati mbaya itatokea ajali", alifafanua mhandisi Andrew.

"Lakini pia mvua zinapunguza ukali wa kemikali hivyo naendelea kuwahakikishia usalama watu wote wanaotuzunguka, tupo vizuri na tumejiandaa vizuri sana kukabili kiashiria chochote cha kuhatarisha usalama katika mgodi wetu", alisisitiza Andrew.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...