Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WANAFUNZI wa kike 15 nchini wamepata ufadhili kamili wa masomo ya shahada ya uzamili katika uhandisi wa nishati endelevu, kupitia mpango unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya sekta ya nishati.

Ufadhili huo umefikisha 60 idadi ya wanawake walionufaika na Mpango wa Ufadhili wa Masomo kwa Wanawake katika Nishati Endelevu (WISE) tangu ulipoanzishwa mwaka 2023.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhi vyeti vya ufadhili na kuzindua awamu ya nne jijini Dar es Salaam,Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu katika Wizara ya Nishati Mhandisi Imani Mruma, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, amesem wanufaika hao watasomea Shahada ya Uzamili ya Uhandisi wa Nishati Endelevu katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Amesema kufanikisha malengo ya Tanzania katika sekta ya nishati kunahitaji wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kubuni na kutekeleza suluhisho la changamoto zilizopo. Hivyo kupitia WISE, wanajenga utaalamu katika nishati jadidifu na ufanisi wa matumizi ya nishati.

“Mpango huu unaunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Ufanisi wa Nishati wa mwaka 2024–2034 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.Programu hii imekuwa na mchango mkubwa kuwawezesha dada zetu kupata ujuzi wa kitaalamu na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya nishati.

“Programu hii imefikia awamu ya nne mwaka huu, ikiwa na jumla ya wanafunzi 60 walioandikishwa katika awamu zote tangu ilipoanzishwa.Ongezeko la idadi ya wanufaika linaonesha mafanikio ya ushirikiano huu na umuhimu wa kuendeleza fursa za elimu ya juu kwa wanawake katika taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.”

Mhandisi Mruma pia ameishukuru Serikali ya Ireland pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT)kwa mchango wao katika kufanikisha programu hiyo, akisema ufadhili wa masomo, miundombinu na vifaa vya kujifunzia vimekuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wake.

Ametoa mwito kwa wanawake wenye sifa kujitokeza kujiunga na programu hiyo, huku akihimiza wafadhili na wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo ili kuongeza idadi ya wataalamu wanawake katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan, amesema ufadhili huo unaakisi dhamira ya nchi yake ya kuimarisha usawa wa kijinsia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwekeza katika elimu na maendeleo ya kitaaluma ya wanawake vijana.

Awali Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) nchini, Shigeki Komatsubara, amesema ufadhili wa masomo ni uwekezaji wa muda mrefu ambao manufaa yake hayaishii kwa wahitimu pekee, bali huenea katika jamii na kuchangia maendeleo ya taifa.

Wakati huo huo Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT)Profesa Preksedis Marco Ndomba, amesema mpango huo unaunganisha elimu ya juu ya uhandisi na mafunzo ya vitendo ili kuwaandaa wahitimu kukabiliana na changamoto halisi za kiufundi katika sekta ya nishati.

Kwa upande wa wanufaika wa mpango huo wamesema fursa hiyo imemwongezea ari ya kuendelea na masomo ya uzamili huku wakiwahimiza wanawake wanaotamani kusomea uhandisi na teknolojia kutoruhusu changamoto za kifedha, kimwili au kisaikolojia kuwazuia kutimiza malengo yao.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...