JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kwa kufanya doria za kubaini na kuzuia uhalifu. Pia oparesheni na misako imeendelea kufanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu wa makosa mbalimbali.
PROGRAMU YA ONGEA NA KAMANDA YAZAA MATUNDA MBEYA.
Septemba 23, 2026 saa 11 alfajiri, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Tumaini John Matimba, mkazi wa Iyela One, Jijini Mbeya alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Iyunga kuwa Pikipiki yake ya Mizigo ya Magurudumu matatu maarufu Guta yenye namba za usajili MC 240 FVV iliyokuwa imeegeshwa katika maeneo ya Iyunga Jijini Mbeya imeibwa na mtu/watu wasiofahamika.
Kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Askari wa Kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu lilianza mara moja ufuatiliaji na ilipofika saa 6:30 mchana liliweza kubaini kuwa Pikipiki hiyo [Guta] iliyoibwa maeneo ya Iyunga ipo maeneo ya Itezi Jijini Mbeya.
Askari pamoja na Mhanga walifika eneo la Mtaa wa Mwasote, Kata ya Itezi, Jijini Mbeya kwenye nyumba moja na kufanikiwa kuikuta Pikipiki ya Mizigo ya magurudumu matatu maarufu Guta yenye namba za usajili MC 240 FVV iliyokuwa imefichwa ndani ya nyumba.
Aidha, katika upekuzi uliofanyika katika nyumba hiyo, zilipatikana mali mbalimbali za wizi ambazo ni Pikipiki moja aina ya Kinglion yenye namba za usajili MC725 ESL rangi nyekundu, Television moja Flat Screen aina ya Alitop nchi 43, Computer moja aina ya Acer rangi nyeusi na Simu Smartphone 15 za aina mbalimbali.
Mali nyingine ni Ving’amuzi viwili, Plate Number 03 za Pikipiki zenye usajili MC 691 FMN, MC 127 DHF na moja namba zake hazisomeki, Spika 2 za Redio aina ya Lg, Stendi 07 za Television, Bracket 25 za kufungia Television ukutani, Begi moja la Spanner mbalimbali pamoja na vifaa mbalimbali vya kuvunjia.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wawili waliokuwepo ndani ya Nyumba hiyo ambao walikimbia muda mfupi kabla ya Askari kufika eneo la tukio.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali na badala yake watafute shughuli halali kwa ajili ya kujipatia kipato halali kwani uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii. Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kufika kituo cha Polisi Mbeya kutambua mali zao walizoibiwa.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...