Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kushughulikia kapu la hoja za ardhi wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, huku ikiwataka wananchi kuhakiki nyaraka za umiliki kabla ya kununua viwanja au mashamba ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, Oktoba 19, 2026, wakati wa Kliniki Maalumu ya Ardhi iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo, Bagamoyo, kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, la kushughulikia changamoto za ardhi katika eneo hilo.

Dkt. Akwilapo amesema miongoni mwa changamoto kubwa ni uvamizi wa maeneo yenye wamiliki halali, akisisitiza kuwa migogoro inayohusu maeneo yenye hukumu za mahakama inapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia maamuzi yaliyotolewa na taratibu za kisheria.

Ameeleza kliniki hiyo inalenga kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi, hususan zinazohusiana na Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo.

Amefafanua kuwa zoezi hilo lililoanza Oktoba 19, 2026, limepangwa kudumu kwa wiki moja, huku muda huo ukiweza kuongezwa kulingana na wingi wa changamoto zitakazojitokeza.

Akizungumzia uendeshaji wa kliniki hiyo, Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nhonge, anasisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa wakati na kuzingatia mahitaji ya wananchi, wakiwemo wazee na watu wenye mahitaji maalumu.

Mbunge wa Bagamoyo, Subira Mgalu, amesema kliniki hiyo itakuwa na manufaa kwa wananchi wenye kero za ardhi, akifafanua kuwa ombi lake lililenga kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto zao, bila kuingilia mashauri ambayo tayari yameamuliwa na mahakama.

Ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza wananchi na Wizara ya Ardhi kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, huku akiwataka wananchi kuheshimu maamuzi ya mahakama na kuepuka hatua zinazoweza kusababisha madhara zaidi, ikiwemo kuvunjiwa majengo yaliyojengwa katika maeneo yenye migogoro.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amewataka wananchi kueleza kwa uwazi kero zao za ardhi, muda zilipoanza na hatua zilizokwisha kuchukuliwa ili kurahisisha utambuzi na utatuzi wake.

Amesema baadhi ya mashauri bado yako mahakamani, hivyo Serikali haiwezi kuingilia maamuzi yaliyokwisha kutolewa, na kuwataka wasiokubaliana na hukumu kufuata taratibu za kisheria.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alitoa agizo hilo Oktoba 16, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kongani ya viwanda ya Kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited) na kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo.








Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Pius Chatanda, amewaomba wananchi wa Kijiji cha Solou, Kata ya Itiso, Wilaya ya Chamwino, kujitokeza kupiga kura Novemba 4, 2026, katika uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Chamwino.

Chatanda ametoa rai hiyo Oktoba 20, 2026, wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wananchi katika mkutano wa ndani uliofanyika kijijini hapo, akiwahimiza kushiriki katika uchaguzi huo na kumpigia kura mgombea wa CCM, Dkt. Nettho Ndijina Ndilito.

Amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi, akieleza kuwa umoja na mshikamano ni mambo muhimu katika kuendeleza dhamira ya chama ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Aidha, Chatanda amewataka wananchi wa Solou kujitokeza siku ya uchaguzi na kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa Jimbo la Chamwino.















MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi karibu na Visiwa vya Ushelisheli umbali wa takribani kilomita 1600 kutoka pwani ya nchi yetu.

Katika taarifa iliyotolewa na TMA Oktoba 20,2026, inasema uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuimarika na kuwa Kimbunga katika eneo la Bahari ndani ya kipindi cha siku nne zijazo na mgandamizo huo unaelekea pwani ya nchi yetu.

"Uwepo wake katika Bahari ya Hindi unatarajiwa kuimarisha kiasi mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu na maeneo jirani hususani kuanzia tarehe 24 Oktoba, 2026." Imesema sehemu ya taarifa hiyo

Aidha, watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa pamoja na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi. Andika title nzuri





WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana na kujadiliana naye masuala ya kilimo, uvuvi na uchumi wa bluu.

Mazungumzo hayo yalifanyika jana (Jumanne, Oktoba 20, 2026) kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue) ulioanza Oktoba 20, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, Marekani.

Katika majadiliano yao, Waziri Mkuu alimshukuru Dkt. Mukeshimana kwa ufadhili unaotolewa na IFAD kwenye uvuvi wa bahari kuu chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na uendelezaji wa uchumi wa bluu kupitia Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi ya Zanzibar.

“Hii miradi ni ya muhimu na inapewa kipaumbele zaidi kwani inasaidia kuzalisha ajira kwa wanawake na vijana,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa IFAD, Dkt. Mukeshimana aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa kitovu cha upatikanaji wa chakula kwa maeneo yanayoizunguka. “Binafsi ninawapongeza kwa sababu mmeendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula cha uhakika barani Afrika. Mnafanya kazi kubwa na nzuri mno ya kulisha chakula kwenye maeneo ya jirani,” alisema.

Kipekee, Dkt. Mukeshimana alimsifu Dkt. Mwigulu akisema: “Tanzania imebahatika sana kupata Waziri Mkuu ambaye zamani alishawahi kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye akawa Waziri wa Fedha. Siyo kila nchi imepata bahati kama hiyo, Tanzania mmebarikiwa sana.”

Alisema taasisi hiyo itaendelea kufadhili miradi inayolenga kuondoa njaa na umaskini kwa kuwekeza kwa watu wa vijijini, kuwezesha ushiriki wao katika masoko na kuimarisha ustahimilivu wa hali ya hewa wa maisha yao.

Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Balozi wa Tanzania Washington, Elsie Kanza na watendaji wengine wa Serikali.









Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya mazungumzo na mshindi wa Tuzo ya Chakula Duniani ya mwaka 2026, Bw. Huub Lelieveld, Oktoba 20, 2026, katika ukumbi wa Iowa Events Center, jijini Des Moines, nchini Marekani.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu amemweleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha sekta ya kilimo. Aidha, amemwambia kuwa watafiti wa kilimo nchini Tanzania wanaendelea kujifunza kutokana na kazi zake ikiwemo uhifadhi wavyakula kwa njia za asili.

Bw. Lelieveld ni mwanasayansi kutoka Uholanzi anayejihusisha na masuala ya usalama wa chakula. Ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2026 na Taasisi ya Tuzo ya Chakula Duniani (World Food Prize Foundation).









▪️ Yashirikiana na Strathmore Business School kuimarisha ujuzi wa uongozi na kuwaandaa wakuu wa idara kushika nafasi za juu zaidi.


Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imeimarisha juhudi za kuandaa viongozi wa baadaye kutoka miongoni mwa wafanyakazi wake, baada ya wakuu wa idara zaidi ya 20 kuhitimu programu maalum ya mafunzo inayolenga kuwaandaa kwa majukumu makubwa zaidi ya usimamizi na uongozi.

Programu hiyo, iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Strathmore Business School, inalenga kuimarisha ujuzi wa kuongoza timu, kusimamia utendaji wa wafanyakazi na kutekeleza mikakati ya biashara. Pia, inawaandaa washiriki kushika nafasi za juu za uongozi, zikiwemo za kiutendaji na za bodi za wakurugenzi.

Akizungumza katika hafla ya mahafali iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Pierre Canton Bacara, alisema kuendeleza uwezo wa wafanyakazi ni muhimu katika kuboresha maamuzi, kuongeza ufanisi wa biashara na kuhakikisha shughuli za kampuni zinakuwa endelevu wakati wa mabadiliko ya uongozi.

“Kadri biashara yetu inavyobadilika, viongozi wetu wanapaswa kuwa tayari kufanya maamuzi magumu, kuongoza timu zao na kufikia malengo. Kuwaandaa kabla ya kuwapa majukumu makubwa zaidi kunawajengea msingi imara na kusaidia kampuni kuendelea na shughuli zake bila kukwama,” alisema Bacara.

Programu hiyo inalenga kujenga kundi la wafanyakazi wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi muhimu za uongozi ndani ya kampuni, huku ikipunguza mapungufu ya ujuzi na kupanua fursa za kuku ana kuendelea kitaaluma. Katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania, kuimarisha uwezo wa uongozi na usimamizi kunaweza kusaidia kampuni kukabiliana na mabadiliko ya soko na kuboresha huduma kwa wateja, biashara na taasisi zinazotegemea huduma za kidijitali.

Mkuu wa Mafunzo na Maendeleo wa Yas Tanzania, Janet Igogo, alisema programu hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni wa kuendeleza rasilimali watu, unaojumuisha mafunzo kwa wakuu wa idara na viongozi wengine waandamizi.

“Nafasi muhimu ndani ya kampuni zinapokuwa wazi, tunataka kuwa na wafanyakazi wenye uwezo wa kushika nafasi hizo. Hili linahitaji maandalizi ya makusudi katika hatua mbalimbali za maendeleo na utendaji kazi wao, kupitia mafunzo yanayowaandaa kwa majukumu watakayokabiliana nayo,” alisema Igogo.

Yas inapanga kuendeleza programu hiyo sambamba na mipango mingine ya kuimarisha ujuzi na uwezo wa rasilimali watu, ili kuongeza idadi ya wafanyakazi walio tayari kushika nafasi za usimamizi na uongozi na kusaidia kampuni kutekeleza malengo yake ya biashara kwa ufanisi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Pierre Canton Bacara (katikati), akifurahi pamoja na wakuu wa idara wa kampuni hiyo wakati wa mahafali yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Zaidi ya wakuu wa Idara 20 walihitimu mafunzo ya uongozi kupitia programu iliyoandaliwa na Kampuni hiyo kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Biashara cha Strathmore.

Wadau wa Uhifadhi nchini wameendelea kuimwagia pongezi kwa hifadhi ya Ngorongoro kutokana na ushindi wa kishindo ilioupata wa kushinda tuzo ya kutukuka ya Ubora katika Utalii Endelevu na Usimamizi wa Uhifadh iliyopokelewa mwishoni mwa wiki jijini Accra, Ghana.


Salamu za pongezi za karibuni zimetolewa na Taasisi ya Uhifadhi na Urithi nchini yenye makao makuu yake jijini Dar essalaam ambapo katika taarifa iliyotolewa na Mtendaji mkuu wa taasisi Costantine Akitanda imeeleza kuwa ushindi wa Ngorongoro ni ushindi wa wadau wote wa Uhifadhi.

“Tuzo hii inathibitisha upya utambulisho wa kudumu wa Ngorongoro kama chimbuko lenye ushahidi kisayansi wa asili ya binadamu, ambapo hatua za kwanza za binadamu zilisikika, uhifadhi endelevu wa urithi wa utamaduni uliopo, mazingira, wanyamapori wakiwa katika mazingira yao ya asili na gunduzi mbalimbali zinaleta upekee kuwa Ngorongoro ni bustani ya Eden iliyotunzwa” imeeleza taarifa hiyo

Taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja na Ngorongoro kuwa sehemu ngumu katika usimamizi kutokana na mfumo wake wa matumizi mseto ya ardhi lakini mamlaka hiyo imeweza kujipambanua katika uhifadhi endelevu

Akizungumza mara baada ya kurejea kutoka Accra, Ghana kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Abdul-Razaq Badru alisema kuwa tuzo hiyo imetokana na ushirikiano wa wadau wote katika mnyororo wa Uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii na kuongeza kuwa wadau wote wana wajibu wa kulinda urithi wake wa kipekee wa asili na utamaduni, huku tukihakikisha kuwa uhifadhi huo unaleta thamani ya kudumu kwa watu, asili na vizazi vijavyo.








Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdi Mahamoud Abdi, amekutana na ujumbe wa viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ambapo wamejadili namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa maendeleo kati ya vyama hivyo viwili.

Kikao hicho kimefanyika katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar, kikijikita katika masuala ya uongozi, miundombinu, biashara, pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Abdi amesema CCM imekuwa na utaratibu wa kuwaandaa viongozi wake kutembelea China kwa ajili ya kujifunza uzoefu wa maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo uongozi na biashara.

Pia, amewapongeza viongozi wa China kwa msaada wanaoendelea kutoa katika Chuo cha Mafunzo cha Dambwe, akieleza kuwa mchango huo una umuhimu katika maendeleo ya chuo hicho.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Zanzibar na China, akieleza kuwa CPC itaendelea kutoa fursa kwa viongozi wa CCM kutembelea China kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na maarifa katika sekta mbalimbali.

Chen amesema maendeleo ya miundombinu ya barabara nchini Tanzania yana mchango katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Khadija Nassor Abdi; Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) CCM Zanzibar, Khadija Salum Ali; Balozi Mdogo Mkuu wa China Zanzibar, Li Qianghua; Mshauri katika Ubalozi wa China nchini Tanzania, Peng Yongjia; pamoja na Katibu wa Pili katika ubalozi huo, Zhang Lianchuang.