
hii imeingia sasa hivi pamoja na hiyo link inayokupa vionjo vya hilo tetemeko. nimeongea na watu wa arusha na moshi wanasema huko viroho juu na habari zinasema jeshi la polisi limewaomba wenye makampuni ya watalii kusitisha kupeleka wageni huko oldonyo lengai. ila hadi sasa hakuna uharibifu wowote ulioripotiwa wala madhara kwa binadamu..
Zaidi ya wafugaji 1,500 wa kabila la Kimasai wamelazimika kukimbia makazi yao wakihofia kuangukiwa na mawe na majabali, baada ya Mlima Oldonyo Lengai uliopo wilayani Ngorongoro wenye volkano hai kulipuka na unaendelea kutoa moshi.
Volkano hiyo imekuja baada ya eneo hilo kukumbwa na matetemeko ya ardhi mfululizo katika siku za karibuni.
Imeelezwa kuwa mlima huo ulianza kutoa moshi na moto, kwa muda wa siku sita sasa na kusababisha uongozi wa vijiji vilivyoko jirani na mlima huo kuwataka waongoza watalii kutowapeleka wageni karibu na mlima huo kwani hali si shwari.
Muongoza watalii wa kupanda mlima huo, Bw. Peter Sule, aliliambia shirika la habari la PST kuwa kwa sasa shughuli za kupanda na wageni juu ya mlima huo zimesimama hadi hali itakapokuwa shwari.
Bw. Sule alisema mlipuko wa sasa wa volkano katika mlima huo ni mkubwa kuliko uliyowahi kutokea, ambapo uliambatana na moshi na moto, hasa nyakati za usiku.
``Kwa kweli hali ya aina hii sijawahi kuiona. Nimeongoza watalii kwa miaka 12 kupanda mlima huo na matukio ya kulipuka kwa volkano yaliyotokea hayakuwa makubwa kiasi hiki,`` alisema Sule.
Aliongeza kwamba nyakati za mchana moshi unakuwa mdogo huku usiku kukiwa na moshi mkubwa ulioambatana na mngurumo.
``Nyakati za usiku ingawa tunaishi mbali na mlima lakini bado tunashindwa kulala kutokana na mtikisiko ambao unatokea mara kwa mara, hii si hali ya kawaida. Hatujui yatakayotokea wakati wowote `` alisema Bw. Sule.
Aidha kiongozi wa ukoo kutoka kwa wafugaji waliokimbia makazi yao karibu na mlima huo, Bw. Loibanguti Kisioki aliiambia PST kuwa katika historia ya maisha yao karibu na mlima huo matukio yasiyokuwa ya kawaida yameanza kutokea katika siku za hivi karibuni.
``Mambo haya ya ajabu ajabu yalianza kutokea miaka michache iliyopita ambapo mwaka jana mlipuko wa volkano ulikuwa mkubwa na umekuwa ukijirudia mara kwa mara,`` alisema Kisioki.
Alisema jamii hiyo imekuwa ikitumia mlima huo kufanya matambiko ya kimila, ``lakini kwa sasa kuna hofu kubwa. Tunahisi Mungu wetu amekasirika ndiyo maana haya yanatokea.``
Aliongeza kuwa wanatarajia kufanya mkutano wa kimila namna ya kumuomba Mungu wao aitwaye Engai Narok awanusuru na balaa linaloweza kusababishwa na tetemeko la mlima huo.``
Wakati huo huo, tetemeko lingine la ardhi lilitikisa Kenya jana.Kutokana na tetemeko hilo, wakazi mbalimbali nchini humo walipatwa na mshtuko mkubwa kufuatia tetemeko la ardhi ambalo lilitokea kwa nyakati mbili tofauti na wengine kukimbia makazi yao.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), tetemeko hilo lilitokea majira ya saa 3.30 na saa 9.30, usiku wa kuamkia jana.
Shirika la BBC liliwakariri maofisa wa hali ya hewa wa Kenya wakisema kwamba tetemeko hilo liliyakumba maeneo yaliyopo katika bonde la ufa.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba hadi jana hakuna taarifa za maafa au majeruhi.
Katika siku za karibuni, mikoa ya Arusha na Kilimanjaro imekuwa ikikumbwa na heka heka kutokana na tetemeko la ardhi. Maeneo ambayo yamepitiwa na tetemeko ni pamoja na Same, Moshi, Longido na Oldonyo Lengai.
Barani Afrika, tukio la volkano linalokumbukwa sana ni lile lilitokea nchini Kongo (DRC) mwaka 1994 baada ya volkano kulipuka katika mlima wa Nyiragongo na kuleta maafa makubwa kwenye mji wa Goma, ulioko umbali wa kilometa 18 kutoka katika kilele cha mlima huo. Mlima huo unapitiwa na Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.
Watalaamu wanasema kuwa volkano hulipuka pale kunapotokea nyufa katika uso wa ardhi na kuruhusu miamba ya ndani ya ardhi iliyoujiuji na yenye moto mkali (molten rock), majivu na gesi kuruka nje.
Ujiuji huo wa moto ukiganda juu ya uso wa dunia unasababisha miamba na shimo linalobakia husababisha ziwa.
Na kuhusu tetemeko la ardhi, watalaamu wanasema linasababishwa na ardhi kuruhusu kwa ghafla nguvu kubwa (stored energy) iliyohifadhiwa ardhini ambayo husababisha mawimbi yaitwayo seismiki.
Wanafafanua kuwa wakati mwingine ni matokeo ya matabaka ya ardhi (tectonic plates) mbayo hutembea na kusababisha mgandamizo mkubwa kwenye ardhi yanaposigishana. Mgandamizo huo unapokuwa mkubwa, husababisha miamba kuvunjika.
Halikadhalika watalaalamu wanasema kwamba wakati matetemeko mengine ya ardhi yanaweza kusababishwa na shughuli za kila siku za banadamu kama vile kupasua miamba, mengine yanatokana na milipuko ya volkano.


Asante sana Michu. Hapo ni karibu kabisa na kijijini kwangu hivyo nategemea wadau wataendelea kutuhabarisha. Blogu hii inasaidia kwa kweli, uongo mbaya! Nimejifunza sana kuhusu tetemeko la ardhi kupitia makala ya Lizzie.
ReplyDeleteKeep it up!!!
Thanx Michuzi
ReplyDeleteLizzie
Shule ya Msingi ya Meigoi iliyopo katika kijiji cha Gilai pamoja na vyanzo vya maji vimeharibiwa vibaya kutokana Volkano iliyotokea juzi katika mlima Oldonyo Lengai.
ReplyDeleteHalikadhalika katika tukio hilo, watoto wawili wameungua vibaya baada ya kumwagikiwa na ujiuji wa moto (lava) uliokuwa ukitoka chini ya ardhi katika mlima huo.
Shule hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300, ina walimu 13 na ina madarasa la kwanza hadi la saba.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Bw. James Milya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo alipokuwa akihojiwa PST katika eneo la tukio.
Alisema kuwa mlipuko huo ulitokea baada ya tetemeko kubwa kuukumba mlima wa Oldonyo Lengai na kusababisha uharibifu mkubwa katika shule ya msingi Meigoi ambapo majengo ya shule hiyo pamoja na nyumba za walimu vimeharibiwa vibaya kutokana na majabali yaliyokuwa yakishuka kutoka katika mlima.
Bw. Milya aliongeza kwamba kutokana na hali mbaya inayoikumba shule hiyo kuna uwezekano wa kuifunga.
Aidha alisema mlipuko huo pia ulisababisha kuanguka kwa mawe ambayo yamesababisha kijiji cha Gilailumbo kukosa maji kutokana na majabali ya mawe kuvifunika vyanzo vya maji na kusababisha wananchi wa kijiji hicho kukosa maji.
``Vyanzo hivyo vilivyofunikwa ndivyo vinavyotoa maji safi katika eneo hilo,`` alisema Bw. James Milya na kuongeza kuwa jitihada za ziada zinahitajika ili kuokoa maisha ya wanakijiji hao.
Kwa mujibu wa wananchi wa kijiji hicho, watu waliojeruhiwa walikuwa wakichota maji kwenye miamba inayouzunguka mlima huo.
Wananchi hao walisema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitumia maji ya mlima huo kwa shughuli mbalimbali za nyumbani na za kilimo.
Aidha habari kutoka katika vijiji vilivyoko jirani na mlima huo, zinadai kuwa baada ya volkano hiyo na tetemeko ambalo lilipita kwa kishindo kikubwa katika vijiji hivyo, hali iliendelea kuwa mbaya kutokana na mitikisiko yenye kishindo kutawala maeneo hayo.
Wananchi hao walifafanua kuwa mtetemo huo wa usiku umesababisha wanyama na ndege waliokuwa wakiishi pembezoni mwa mlima huo kuhama kutokana na hali hiyo.
Ndege waliohama eneo hilo ni wale ambao husafiri kutoka Ulaya kutokana na kukimbia baridi kwenda eneo hilo kuzaa na kusubiri kipindi cha baridi halafu wanarudi Ulaya.
Wananchi hao waliiomba serikali kuwa na chombo kitakachokuwa kikitoa taarifa za matukio ya hatari kama hayo ili watalii na wananchi wasidhurike na majanga kama hayo.
Wakati huo huo, Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Bw. Jowika Kasunga alisema hawajapa taarifa rasmi ya madhara ya volkano hiyo pamoja na tetemeko na kuongeza kwamba uchunguzi unafanyika ili kujua athari za volkano hiyo katika vijiji vinavyozunguka mlima huo.
Akizungumza na BBC jana jioni, Mtaalamu wa Jiolojia kutoka Pretoria, Afrika ya Kusini, Profesa Sospiter Muhongo, alisema mlipuko wa volkano hauwezi kutokea kama hakuna tetemeko, hivyo ili volkano itoke juu ya ardhi ni lazima kuwepo na tetemeko ambalo litapasua miamba na kutengeneza nyufa ambazo zitaruhusu volkano kutokea.
Alisema ujiuji wa volcano (lava) unaotoka katika mlima Oldonyo Lengai haupatikani sehemu nyingine duniani, kutokana na ujiuji wa mlima huo kuwa mweupe.
Alifafanua kuwa lava zinazotoka katika milima mingine kama ya Meru, Kilimanjao na mingine duniani huwa ni nyeusi.
Wakati huo huo, Serikali imetoa ushauri kwa wananchi kuingia uvunguni mwa meza ama vitanda na kubakia hapo kwa muda pindi wanapohisi kuwa na tetemeko.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini, (TMA), Dk. Mohammed Mhita alisema katika taarifa yake kuwa wananchi wanatakiwa kukaa mbali na maeneo yenye moto na vitu vizito.
``Unashauriwa kuwa mwangalifu wakati unakimbia kutoka nje ya jengo na kutelemka kwenye ngazi. Upo uwezekano wa kuangukiwa na mabaki ya jengo kama vioo na tofari,`` alisema.
Aliongeza iwapo upo nje, unashauriwa ukae maeneo ya wazi mbali na majengo, miti na nyaya kwani vinaweza kukuangukia na kuhatarisha maisha yako.
Alisema kwa wanaoendesha magari wanashauriwa kuyasimamisha pembezoni mwa barabara kwa uangalifu na kubaki ndani ya gari hadi tetemeko liishe.
�Ukiwa kwenye maeneo ya milima uwe mwangalifu na mawe yanayotelemka na vitu vingine vinavyoweza kutikiswa,� alisema.
Alisema matarajio ni kuwa matetemeko yatakayoendelea kuwepo yatakuwa katika kiwango ambacho hakitaleta madhara na hivyo wananchi kuendelea na shughuli zao za kawaida.
Juzi, zaidi ya wafugaji 1,500 wa kabila la Kimasai walilazimika kuyahama makazi yao kwa kuhofia kuangukiwa na majabali yaliyokuwa yakiporomoka kutoka katika mlima Oldonyo Lengai baada ya volkano kulipuka.
Volkano hiyo imelipuka baada ya eneo hilo kukumbwa na tetemeko la ardhi mfululizo.
Mlima Oldonyo Lengai ulianza kutoa moshi kwa siku sita kabla ya volkano hiyo kulipuka ambapo viongozi wa vijiji vilivyopo jirani na mlima huo waliwataka wananchi wao kuyahama maeneo yao kwa muda ili kuokoa maisha yao.
Volkano ya mlima huo iliyotokea juzi imeelezwa kuwa kubwa na ya aina yake katika kipindi cha miaka 12.