KIUMBE ADIMU AMBAYE JAPO AMEKUFA SAUTI YAKE NA MATENDO YAKE YANAENDELEA KUTOA CHANGAMOTO CHANYA KATIKA MAISHA YETU WANA-MARA NA TAIFA ZIMA KWA UJUMLA.

Siku kama ya leo, mwaka mmoja uliopita makucha ya kifo pasipo huruma wala taarifa yalituondolea pumzi ya uhai ya Mzee wetu Amos Mutaragara Chirangi wa Muhongo wa Nyawayega wa Rihu. Marehemu mzee Chirangi aliyezaliwa mwaka 1932 huko Bushora Mwirengo Mugango, Mkoani Mara, aliacha alama za kishujaa kama Kiongozi, Mzalendo na Muumini wa kuigwa katika kizazi hiki na vijavyo.
Familia ya Chirangi inawashukuru sana wananchi wote wa Mkoa wa Mara na kwingineko, Serikali yetu, Jumuiya zote za Kidini, CCM na Vyama vyote vya siasa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi na Asasi mbalimbali za kijamii kwa Faraja, Misaada mbalimbali, Umoja na Mshikamano wao waliotuonyesha wakati wa msiba hadi huduma za mazishi za marehemu baba yetu Mutaragara Chirangi. Kila mwaka familia yake itakuwa inaainisha dhamira moja kuu ambayo inaakisi moja ya sifa zake kama changamoto kwetu. Mwaka huu tunaanza na sifa yake ya UWEKAJI MIPANGO (Planning):-

Alikuwa mtu wa kuandaa mambo yake barabara kwa wakati muafaka na kwa kiwango kinachoridhisha hivyo akaitwa ‘Mzee wa Standard’. Ni mzee aliyepinga kwa vitendo uongozi na maisha ya ‘uzima moto’, ndiposa tulishuhudia hata akiwa amejiandalia mapema wosia kwa familia na kaburi lake mwenyewe kwa zaidi ya miaka kumi sio kwa udhoofu wa afya yake bali kwa msingi wa kujiandaa na kutotaka kusababisha usumbufu wowote kwa jamii wakati anajua kuwa kauli ya Mungu pale Edeni kuwa ‘hakika mtakufa’ ni ya kweli na kwamba ilimuhusu pia hata na yeye.
Ni mzee aliyekuwa rafiki wa karibu wa nyenzo KALENDA si kwa sababu ya kujua jinsi siku zinavyokwenda bali zaidi kujipanga katika siku zinavyokuja.
Tunapoanza mwaka mpya 2008 sauti ya mzee Chirangi inatuasa sote kuwa tuwe watu wa mipango na utekelezaji. Tuweke mipango yetu ya muda mfupi na mrefu popote tulipo iwe ni katika familia, au katika Chama au Taasisi au Kampuni au Usharika, au Jumuiya yeyote kwa ajili ya maendeleo yetu. Maana ni kweli kuwa usipojua unapoelekea kamwe huwezi kupotea maana popote utakapokuwa utafikiri kuwa umefika.


Waweza pia kupitia blogu yenye anuani;

http://hakihuinuataifa.blogspot.com/
kwa habari zaidi za mzee Chirangi na familia yake.

KWA HESHIMA NA SHUKRANI,
FAMILIA YA CHIRANGI INAWASILISHA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Jamani ni kweli huyu mzee hakuwa mchezo. Pamoja na kuwa CCM-damu bado wakati wa mazishi yake Kiongozi wa upinzani alisimama a kutamka waziwazi kuwa huyu mzee anastahili kutangazwa na kutunukiwa na serikali kuwa kiongozi wa mfano aliyepigana na rushwa kwa maneno na matendo! du kweli kila aliyewahi kutana naye anajua hili.

    ReplyDelete
  2. Poleni sana. Ni kweli msimamo wa huyu mzee Standard ulikuwa si wa kawaida. Aliwahi pelekewa fedha za ili amkampeinie mpinzani wa JK wakati wa mchakato wa awali wa urais ndani ya CCM, akawatoa puta hao jamaa na burungutu lao. Stori hii aliisema mwenyewe hadharani na pia inajulikana Musoma.

    ReplyDelete
  3. MICHUZI nimequote haya maneno ya huyu mzee Chirangi kutoka kwenye hiyo blogu yake ili yahubiriwe kokote hata huko Kenya kwa wenzetu watu watulie.

    "Kama ambavyo nimekuwa nikisema na kutenda, ieleweke wazi kuwa kiongozi achaguliwaye kwa kutoa fedha, ataongoza kwa kuchukua fedha, vilevile achaguliwaye kwa kufuata ukabila, atasimamia kabila, naye yule achaguliwaye kwa kampeni moto toka juu huenda akaondolewa kwa kampeni baridi kutoka chini. Aidha, ni kitendo cha kutokukomaa kisiasa, kujenga chuki na hasira kwa mtu yeyote eti kwa sababu ya kutokupigia kura, kukushinda kwenye uchaguzi au kuazimia kugombea nafasi uliyodhani umetengewa wewe pekeke".

    Alikuwa mzee wa shoka huyu.

    mdau

    ReplyDelete
  4. RIP mzee Amos,
    Our nation remembers yours contributions from the 50's to the 2000's in education, sports & games, labour movements, politics and in religious organisations.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...