Assalam alaykum na habari za mwisho wa wiki wadau.
Kaka issa na wadau, yakhe mi nimefurahishwa sana na mwamko wa Watanzania na walimwengu kwa ujumla juu ya matumizi ya Kiswahili, lugha yetu mama, lugha yetu pendwa, hazina pekee iliyobaki ya kujivunia.
Wiki iliyopita kaka Chibiriti aliomba msaada wa kupatiwa methali au misemo 12 ya Kiswahili. Alhamdulillah alipata zaidi ya kumi na mbili.
Hii inaonesha ni kiasi gani Waswahili wanakithamini Kiswahili chao, ingawa kwa lahaja na lafudhi tofauti, lakini bado ni chetu na twajivuniacho. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba viongozi wetu hawaoneshi kimatendo kuthamini kwao Kiswahili chetu.
Nasema hili kwa ushahidi huu: mara nyingi viongozi wetu wanapofanyiwa mahojiano na vyombo vya habari vya kimataifa kwa lugha ya Kiswahili wao hujibu kwa kiingereza, labda kuonesha kwamba wao hawako nyuma katika umahiri wa lugha za watu.
Kwangu mimi, naamini na kwa wazalendo wengine, hili si la kujivunia! Kinachouma zaidi ni pale tunapowasikia viongozi wa nchi jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo na kadhalika ambao sisi ndio tumewapelekea hicho Kiswahili, wao wanapofanyiwa mahojiano kwa Kiswahili basi hujilazimisha kuzungumza Kiswahili japo kimagube lakini kuonesha wanathamini Kiswahili kuliko hata lugha zao za asili.
Pia mara nyingi unapokwenda katika balozi zetu ughaibuni utakuta fomu na maelezo mengine kadhaa yameandaliwa kwa kiingereza na lugha ya nchi hiyo husika, bali hukuti lugha ya Kiswahili. La kujiuliza ni je zile balozi zetu pamoja na kuweka mahusiano na mawasiliano mazuri na nchi marafiki, lakini si pia zinatakiwa kutuhudumia sisi wananchi wake? Au ndio wao huchukulia kiurahisi kwamba watu wote kwa kuwa wako ughaibuni watakuwa wanazungumza kiingereza au hizo lugha nyingine? Hilo mimi nahisi sivyo, na si la kujivunia! Wenzetu wanaothamini lugha zao hupa vipaumbele lugha zao kwanza ndipo hufuatia nyingine.
Watanzania tumezowea kujiachia na kuporwa hazina zetu kiholela. Tumesikia kwamba mlima Kilimanjaro ni mali ya Kenya. Viongozi kimyaaa! Wananchi ndio kifua mbele. Na hadi leo hii bado wageni wengi ambao hawajafika Tanzania wanaamini kuwa mlima Kilimanjaro upo na ni mali ya Kenya. Nakhofishwa kwamba hata na hicho Kiswahili sasa kinakaribia kuwa mali ya haohao Wakenya kwa sababu wao hujitangazia kuwa ni lugha ambayo imechimbukia kwao.
Wao hujitangaza na kujitafakhari kwacho, ilhali sisi, hususan viongozi wetu, twakipiga pute. Wito kwa viongozi na watanzania kwa jumla tukienzi na kujifaharisha kwa Kiswahili chetu. Lugha yetu ni nzuri na ina ladha ya aina yake ukiijua vitakiwavyo. Ningeomba tutumie kila nafasi tuipatayo kwa kujitangaza kwa Kiswahili chetu.
Kutumia Kiswahili kwenye mahojiano au mikutano ya kimataifa ni nafasi nzuri ya kusema kuwa Kiswahili ni lugha yetu na tunaipenda. Na haitapunguza mshahara wenu waheshimiwa.
Kitangaze Kiswahili upate kutambulika
Kiseme kiumahiri wala usiwe na shaka
Lafudhiye ni sahili raha ukikitamka
Sikiache ‘kahajiri ’takuja baki wabweka!
Wakatabahu,
Mzanzibari DK.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Mdau uliyeleta hii mada nakuunga mkono kwa vidole vyote kumi ningekuwa na mikono ishirini pia ningefanya hivyo.Sisi Watanzania tunashangaza sana hatunyamini si kiswahili tu bali vitu vyingi vitokavyo kwetu.Ni ajabu sana.Nadhani watanzania tunasumbuliwa na kuwa na "low self esteem",ndio maana tunang'ang'ania vya wenzetu na kuona vyetu ni vibaya.Pia wabongo tunakuwa na wasiwasi/woga wa jinsi tutakavyoonekana kwa wengine.Ni kinyume na mataifa mengine wao hawajali wapo wapi na nani anawaangalia.Huku kwa nchi za wengine Waafrika watokao kama liberia,nigeria nk wao bwana hawajali cha mtu,wanaongea lugha zao popote pale na inapokuja maswala mengine kama kubeba mtoto mgongoni wanafanya hivyo hivyo kama wako "upoponi". Sijawahi kuona Mtanzania anafanya hivyo.Mtanzania akiwa mbele za wengine utamwona anaona aibu kuongea kiswahili ni ajabu sana.Sijui huu ugonjwa utaondoka lini.
    *samahani kwa kutumia lugha ya wengine(Low self-esteem)

    ReplyDelete
  2. MDAU HATA MIMI NAKUUNGA MGUU KWANI VIONGOZI WETU WENGI NI MALIMBUKENI WA LUGHA ZA KIGENI NA HATA SISI BAADHI YETU NI MALIMBUKENI KWANI KUNA MSHIKAJI WANGU MMOJA ANA NDUGU YAKE YUPO UHOLANZI BASI AKIMPIGIAGA SIMU ANAMSEMESHESHA KIHOLANZI SASA YULE YULE MSHIKAJI WANGU ANAKUWA AMUELEWI NDUGU YAKE SASA HUO SI ULIMBUKENI? MTU ANAISHI BONGO AJAWAHI KUSOMA KIHOLANZI WALA HAJAWAHI KWENDA HUKO UNAMSEMESHA KILUGHA CHA HUKO NA KUHUSU WAKENYA KWELI WATATUACHA SASA HIVI KAMA WALIVYOUCHUKUA ML KILIMANJARO KIBIASHARA. NA KUNA WAKATI NILIWAHI KUTEMBELEA BALOZI ZA RUSSIA.SIRYA NA BULGARIA HAPA BONGO NIMEANGALIA FOMU ZAO ZA MAOMBI YA VIZA HAKUNA HATA MOJA ILIOANDIKWA KISWAHILI ZOTE ZIMEANDIKWA LUGHA ZA KWAO SASA KWANINI? ZETU ZISIANDIKWE KISWAHILI
    MDAU
    KISIJU PWANI

    ReplyDelete
  3. Kuhusu viongozi wetu kutothamini kiswahili, ni kweli. Nilitokwa mchozi wa furaha na huzuni pale Chisano alipotumia lugha ya Kiswahili fasaha na kwa kujiamini kuhutubia mkutano wa AU.

    Simanzi na ghadhabu zilinijia kwa vile kabla Raisi wetu Benjamin Mkapa kwa mbwembwe alipohutubia mkutano huo huo kwa kingereza apmoja na umahiri wake wake wa kukijua kiswahili na kutunga maneno kama vile 'mbadala' 'tegemezi' utanda-wazi, endelevu nk

    Niliwahi kusikia kuwa kwa umahiri wake akiwa Mhariri wa Nationalist aliwahi pia kuwa mwandishi wa Raisi wetu wa mwanzo. kwa hiyo sio tu anankiongea bali pia kukiandika kiswahili vizuri. Kwa hiyo alipenda hata mahijiano na waandishi kwa kizungu kama vile na Tim Sebastian au Riz Khan na sio na kina Mzee Je Tutafika!!

    ReplyDelete
  4. wewe anon wa 3 12:41 ALIEKWAMBIA MKAPA KATUNGA HAYO MANENO NANI? - UTANDAWAZI,MBADALA,ENDELEVU NA TEGEMEZI. wa wapi wewe?he! embu acha kuongea pumba.maneno hayo yamechapishwa kwenye kamusi tokea miaka ya 60,we unakuja kusema eti mkapa kayatunga. atambe?

    ReplyDelete
  5. DK nakubaliana na wewe, angalia watu wanaoishi Ulaya hawawafundishi watoto kiswahili, wanaona raha wakirudi bongo,kusikia mtoto wa ----- anaporomosha umombo hatari hajui hata kiswahili, ushamba kwelikweli, angalia mfaransa, mwingereza, mjerumani na mataifa mengine wakiishi Bongo lazima watoto wao watajua lugha za kwao,wakirudi makwao hawapati tabu,jamani tuache ushamba. BUSH QUEEN

    ReplyDelete
  6. Mnao kaa nje nchi ni vizuri muache ushamba, hayo mambo ya kutowafundisha watoto kiswahili yamepitwa na wakati, mtoto akiwa mdogo anaweza kushika hata lugha tatu kwa wakati mmoja.

    ReplyDelete
  7. Jamani kuna mama mmoja simtaji jina,lakini ukoo wake ni wa kina Amri pale Dar,kama huwajui basi wewe mgeni,huyo mama anakaa Uholanzi,watoto wake wanazungumza Kiswahili, Kidachi, Kifaransa,na Kingereza, kwa hiyo hata wakirudi leo wanataka kugombea ubunge wa Mahenge wanaweza kupata, kuliko yule anayerudi hajui lugha,ataelewana vipi na watu wajimboni kwake. Bush Queen

    ReplyDelete
  8. MYSELF NIKIONGEA OR READ KISWAHILI I GET A HEADACHE, I DON'T KNOW ABOUT OTHERS.

    ReplyDelete
  9. Ushamba unakuangaisha, na utumwa unaupenda kwelikweli,wewe angea kingereza upendavyo lakini bado unakuwa mbongo tu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...